Rais Rouhani: Umoja wa Wairani umewezesha kushinda njama za Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i58780-rais_rouhani_umoja_wa_wairani_umewezesha_kushinda_njama_za_marekani
Rais Hassan Rouhani amesema, Marekani ilijitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na ikamuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kutaka Iran itengwe, hata hivyo umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran umewezesha kushindwa na kugonga mwamba njama hizo za Marekani.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 27, 2020 08:55 UTC
  • Rais Rouhani: Umoja wa Wairani umewezesha kushinda njama za Marekani

Rais Hassan Rouhani amesema, Marekani ilijitoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na ikamuua kigaidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, kamanda wa kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kutaka Iran itengwe, hata hivyo umoja na mshikamano wa wananchi wa Iran umewezesha kushindwa na kugonga mwamba njama hizo za Marekani.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kongamano la magavana na wakuu wa mikoa nchini. Ameashiria ukuaji uchumi wa Iran katika eneo la Asia Magharibi na akasema: Baada ya maadui kushuhudia nguvu za wananchi na kustawi uchumi wa Iran wanalenga kuuvunja mshikamano, umoja, utulivu na uchumi wa wananchi wa Iran.

Rais Rouhani ameashiria pia uchaguzi wa 11 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) utakaofanyika tarehe 21 Februari na akasisitiza kwamba: Mahudhurio ya wananchi wa Iran katika medani mbali mbali yamekuwa ndio wenzo wa nguvu na uwezo wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu.

Wananchi wa Iran wakishiriki katika moja ya chaguzi nchini

Huku akiashiria kwamba Jamhuri ya Kiislamu si ya mfumo wa chama kimoja, Rais Rouhani amesema: Katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran matabaka yote kutoka mirengo tofauti yanashiriki pamoja katika uchaguzi.

Uchaguzi wa 11 wa Bunge la Iran utakaohusisha majimbo 208 ya ubunge kwa ajili ya kuchagua wawakilishi 290 wa bunge nchini kote pamoja na uchaguzi mdogo wa baraza la tano la wanazuoni wataalamu wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya majimbo matano ya Tehran, Fars, Khorasan Kaskazini, Khorasan Razavi na Qum utafanyika tarehe 21 ya mwezi ujao wa Februari.../