Mar 05, 2020 13:25 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: India isitishe mauaji ya Waislamu iwapo haitaki kutengwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitahadharisha serikali ya India dhidi ya kuendelea kutekeleza mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa, ukandamizaji unaoendelea kufanyiwa Waislamu katika nchi hiyo ya kusini mwa Asia utapelekea serikali ya New Delhi itengwe katika ulimwengu wa Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo Alkhamisi katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwa lugha za Kiurdu, Kiingereza na Kifarsi ambapo amelaani vikali mauaji ya makumi ya Waislamu katika ghasia zinazoendelea kushuhudiwa katika mji mkuu wa India, New Delhi tokea Februari 23. 

Katika ujumbe huo, Ayatullah Khemenei amesema, "nyoyo za Waislamu wote kote duniani zinaomboleza na kusikitika kutokana na mauaji ya halaiki ya Waislamu nchini India."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaka serikali ya India ipambane na Wahindu wenye misimamo mikali na vyama vyao, na kukomesha mauaji ya Waislamu ili kuzuia India isitengwe katika ulimwengu wa Kiislamu. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amemalizia ujumbe huo kwa kutumia alama ya reli (hashtegi) na kuandika #WaislamuWaIndiaKatikaHatari.

Waislamu wa India katika maandamano ya kulaani sheria ya kibaguzi

Siku ya Jumatatu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Mohammad Javad Zarif alisema Jamhuri ya Kiislamu inalaani vikali ukatili na ghasia zilizoratibiwa dhidi ya Waislamu nchini India, akisisitiza kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro uliopo ni kufuata sheria na mazungumzo ya amani.

Hivi karibuni Bunge la India linalodhibitiwa na Wahindu wenye misimamo mikali lilipasisha sheria ya kibaguzi ambayo imesababisha machafuko makubwa na hadi sasa watu 43 wameuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika ghasia zilizosababishwa na sheria hiyo iliyo dhidi ya Waislamu nchini humo.

 

 

Tags