Iran: Uropokaji mpya wa Marekani unakusudia kuipotosha dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60468-iran_uropokaji_mpya_wa_marekani_unakusudia_kuipotosha_dunia
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani imeazimia kuupotosha ulimwengu, ili usishughulishwe tena na ugaidi wa kiuchumi wa taifa hilo la kibeberu dhidi ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 19, 2020 03:22 UTC
  • Iran: Uropokaji mpya wa Marekani unakusudia kuipotosha dunia

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani imeazimia kuupotosha ulimwengu, ili usishughulishwe tena na ugaidi wa kiuchumi wa taifa hilo la kibeberu dhidi ya Iran.

Majid Takht-Ravanchi ameyasema hayo katika radiamali yake kwa bwajabwaja mpya za Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo kuhusu vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.

Mwanadiplomasia huyo wa wa ngazi za juu wa Iran ameandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuwa: jaribio jingine la Marekani la kupotosha, mkabala wa muendelezo wake wa ugaidi wa kiuchumi dhidi ya taifa la Iran. Mara hii, Marekani inalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likiuke azimio lake lenyewe nambari 2231, na liendelee kuiwekea Iran vikwazo vya silaha.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza bayana kuwa, sera za Marekani kuhusu Iran hazina muelekeo na kwamba Washington itagonga mwamba katika jitihada zake za kuziburuza nchi nyingine duniani zikiuke sheria za kimataifa kama inavyofanya yenyewe.

Kikao cha Baraza la Usalama la UN

Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter jana Jumamosi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo alidai kuwa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa sharti lirefushe muda wa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Hii ni katika hali ambayo, baada ya kusainiwa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, Baraza la Usalama la UN lilipaswa kuiondolewa Iran vikwazo vya silaha mnamo Oktoba 18 mwaka huu 2020, baada ya Wakala wa Kimataifa wa Niashati ya Atomiki IAEA kutathmini na kuthibitisha malengo ya amani ya miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu.