Apr 26, 2020 02:43 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Kutomuogopa adui, ni katika mafundisho muhimu ya Qurani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kutomuogopa adui na kusimama kidete dhidi yake ni katika maamrisho na maelekezo muhimu ya Qurani Tukufu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo jana Jumamosi katika marasimu ya kisomo cha Qurani katika siku ya kwanza ya mwezi mtukufu wa Ramadhani nchini katika ukumbi wa Musalla wa Imam Khomeni hapa jijini Tehran na kuongeza kuwa: Hii leo, hali ya kudhalilishwa baadhi ya mataifa ya Kiislamu na madola ya kidhalimu duniani imetokana na kuogopwa maadui wa Uislamu.

Kiongozi Muadhamu amefafanua kuwa, "kuigopa Marekani kuna matokeo machungu, na haya tumeyashuhudia katika miaka ya nyuma, ambapo mwenendo wa baadhi ya viongozi wetu kuiogopa Marekani kuliwasababishia matatizo."

Amesema, "njia pekee ya kuinusuru jamii ya wanadamu kuondokana na dhulma, ubaguzi, maonevu, vita, ukosefu wa usalama, na kutoheshimiwa thamani za kiutu ambako kumeshuhudiwa katika kipindi chote cha historia, ni kufuata kivitendo mafundisho ya Qurani Tukufu."

Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa,  Qurani ni kitabu cha maisha, na iwapo wanadamu watashikamana na sheria zake, bila shaka watapata baraka na ufanisi hapa duniani na kesho Akhera.

 

Kiongozi Muadhamu akiomba dua

Ayatullah Khamenei ameeleza bayana kuwa, iwapo sheria za maisha ya dunia zitajengeka katika misingi ya uchu wa kusaka nguvu, fedha na matamanio, basi mwanadamu hatopata saada na furaha katika maisha ya dunia na ya kesho Akhera.

Amebainisha kuwa, Qurani Tukufu imemfudisha mwanadamu kutumia utajiri na uwezo wake wote kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wanadamu wenzake, na kuwasaidia watu wenye mahitaji katika jamii.

Kadhalika Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kutoa mkono wa kheri na fanaka kwa Waislamu wote kote duniani kwa mnasaba wa kuanza mwezi mtukufu wa Ramadhani, ameuasa umma wa Kiislamu kustafidi na mwezi huu kwa kujikurubisha zaidi kwa Mola, kwa lengo la kuwanusuru walimwengu wote.

 

 

Tags