Zaidi ya wagonjwa 78 elfu wa COVID-19 wamepona nchini Iran
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa 78 elfu na 422 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran alitangaza hayo jana Jumapilii katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 976 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia jana adhuhuri watu 97,424 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.
Daktari Jahanpur hali kadhalika ameashiria kufariki dunia wagonjwa 47 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,203 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.

Idadi ya walioambukizwa corona duniani kote hadi sasa ni zaidi ya milioni 3.5 ambapo watu wasiopungua 245,000 wameaga dunia na wengine zaidi ya milioni moja wametibiwa na kuruhusiwa kuondoka hospitalini.