Zaidi ya wagonjwa 83 elfu wa COVID-19 wamepata nafuu nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60863-zaidi_ya_wagonjwa_83_elfu_wa_covid_19_wamepata_nafuu_nchini_iran
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa 83 elfu na 837 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
(last modified 2026-07-02T04:13:23+00:00 )
May 08, 2020 19:32 UTC
  • Zaidi ya wagonjwa 83 elfu wa COVID-19 wamepata nafuu nchini Iran

Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa 83 elfu na 837 wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata nafuu na afya njema na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran alitangaza hayo jana Ijumaa katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 1,556 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia jana adhuhuri watu 104,691 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.

Mgonjwa wa COVID-19 akipata matibabu Iran

Daktari Jahanpur hali kadhalika  ameashiria kufariki dunia wagonjwa 55 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia jana adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,541 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.

Idadi ya walioambukizwa corona duniani kote hadi sasa ni zaidi ya milioni 4 ambapo watu wasiopungua 270,000 wameaga dunia na wengine zaidi ya milioni moja na laki tatu wametibiwa na kupata nafuu.