Waliopona ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran ni zaidi ya 85,000
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60875-waliopona_ugonjwa_wa_covid_19_nchini_iran_ni_zaidi_ya_85_000
Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa zaidi ya 85 elfu wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 09, 2020 08:06 UTC
  • Waliopona ugonjwa wa Covid-19 nchini Iran ni zaidi ya 85,000

Wizara ya Afya, Matibabu na Mafunzo ya Tiba ya Iran imetangaza kuwa, hadi hivi sasa waathiriwa zaidi ya 85 elfu wa ugonjwa wa COVID-19 au corona humu nchini wamepata afueni na kuruhusiwa kurejea nyumbani kutoka mahospitalini.

Daktari Kianoush Jahanpour, Mkuu wa Idara ya Mawasiliano ya Umma na Upashaji Habari ya Wizara ya Afya ya Iran amesema hayo leo katika kikao cha kila siku na waandishi habari na huku akigusia kugunduliwa watu wapya 1,529 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi cha masaa 24 nchini Iran amesema, hadi kufikia sasa watu 106,220 walikuwa wamethibitishwa kupata ugonjwa wa corona humu nchini.

Kadhalika  ameashiria kufariki dunia wagonjwa 48 wa corona nchini Iran katika kipindi cha masaa 24 hadi kufikia leo adhuhuri na kusema kuwa, hadi hivi sasa watu 6,589 wameshafariki dunia kwa COVID-19 humu nchini.

Vifaa vya kupima corona vilivyotengenezwa na wataalamu wa Iran

Wakati huohuo, Iraj Harirchi, Naibu Waziri wa Afya wa Iran amesema idadi ya watu wanaoaga dunia kwa ugonjwa wa Covid-19 na kadhalika wanaoambukizwa maradhi hayo imepungua kwa kiasi kikubwa katika mji mkuu Tehran katika wiki za hivi karibuni.

Katika hatua nyingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Muhammad Javad Zarif amesema nchi hii imetuma vifaa vya kupima virusi vya corona zaidi ya 40,000 katika nchi kadhaa duniani kama vile Ujerumani na Uturuki.