Rouhani: Jamii ya kimataifa inapaswa kukomesha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i60986-rouhani_jamii_ya_kimataifa_inapaswa_kukomesha_jinai_za_israel_dhidi_ya_wapalestina
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha jinai dhidi ya binadamu, ukandamizaji na dhulma wanazofanyiwa Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 14, 2020 19:59 UTC
  • Rouhani: Jamii ya kimataifa inapaswa kukomesha jinai za Israel dhidi ya Wapalestina

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua za kivitendo za kukomesha jinai dhidi ya binadamu, ukandamizaji na dhulma wanazofanyiwa Wapalestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais Rouhani alisema hayo jana Alkhamisi kwa mnasaba wa siku ya "Nakba" yaani siku ya nakama ya kuasisiwa utawala pandikizi wa Israel katika ardhi walizoporwa Wapalestina na kubainisha kuwa, "Israel inapaswa kulazimishwa kuondooka katika ardhi za Wapalestina inazozikalia kwa mabavu."

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds ya mwaka huu, Dakta Rouhani amesema, "katika hali ambayo siku hii ya kulaani utawala ghasibu wa Israel na kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina ni muhimu na inayopaswa kubakishwa hai, lakini protokali za kiafya zinapaswa kuzingatiwa pia."

Huku akishiria kuwa vyombo vya habari vina nafasi muhimu ya kuakisi dhulma wanazofanyiwa Wapalestina na utawala haramu wa Israel, Rais wa Iran ameeleza bayana kuwa, "tunapaswa kuchukua hatua za kuulaani utawala wa Kizayuni wa Israel na kuonyesha uungaji mkono kwa wananchi wa Palesatina kwa kutumia njia na mbinu athirifu zaidi kuliko miaka ya huko nyuma."

Matembezi ya Siku ya Quds mjini Tabriz nchini Iran mwaka uliopita

Imam Khomeini MA Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza kuwa Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni Siku ya Kimataifa ya Quds. 

Waislamu na wapenda haki wamekuwa wakifanya maandamano katika pembe mbalimbali za dunia kila mwaka katika Siku ya Kimataifa ya Quds, na kubainisha hasira zao kwa siasa za kibaguzi na kikatili zinazotekelezwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina. Hata hivyo kutokana na janga la corona, maadhimisho ya mwaka huu yanatazamiwa kufanyika zaidi mubashara kwenye mitandao ya kijamii.