Shamkhani: Kuvunjwa 'masanamu ya kibaguzi' kumewatia kiwewe Wazayuni
-
Ali Shamkhani
Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kitendo cha kuvunjwa nembo na masanamu yanayoashiria ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani kimeutia kiwewe na wahka mkubwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ali Shamkhani amesema hayo katika ujumbe alioutuma jana Ijumaa kwenye ukurasa wa Twitter na kubainisha kuwa, "dunia imesikia sauti ya wanaodhulumiwa baada ya kupita karne kadhaa, na labda utawala wa kibaguzi na Kizayuni una wasiwasi mkubwa kuliko utawala wowote ule kutokana na kuvunjwa nembo za ubaguzi Magharibi."
Amesema Wazayuni wana wasiwasi mkubwa kwa kuwa wanafahamu vyema kuwa, baada ya kuvunjwa masanamu ya kibaguzi katika nchi za Magharibi, utawala huo wa Kizayuni watafuata.
Waandamanaji wenye hasira nchini Marekani na maeneo mengine duniani wanaendeleza mkakati wa kuangusha, kuharibu na kuondoa masanamu ya wabaguzi wa rangi. Katika miji mbalimbali ya Marekani waandamanaji wameendelea kuvunja masanamu ikiwa ni pamoja na sanamu la Christopher Columbus, mzungu kutoka Ulaya aliyedai kuvumbua bara Amerika na sanamu la Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa, katika karne ya 17.
Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani wamebomoa, kuharibu na kuvunja vichwa vya sanamu la Christopher Columbus kuanzia miji ya Boston upande wa kaskazini hadi Miami huko kusini. Wanasiasa mbalimbali nchini Marekani wametoa wito wa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki watumwa baada ya maandamano yaliyochochewa na kifo cha George Floyd wiki tatu zilizopita.
Mbali na Marekani, wimbi hilo la kuvunjwa masanamu na nembo hizo zinazoashiria ubaguzi wa rangi linashuhudiwa katika nchi kadhaa duniani hususan za Ulaya.