Rouhani: Iran ina uhusiano mzuri na nchi jirani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i62082-rouhani_iran_ina_uhusiano_mzuri_na_nchi_jirani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran ina uhusiano mzuri na nchi jirani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 08, 2020 11:35 UTC
  • Rouhani: Iran ina uhusiano mzuri na nchi jirani

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema Iran ina uhusiano mzuri na nchi jirani.

Akizungumza Jumatano katika kikao cha Baraza la Mawaziri mjini Tehran, Rais Rouhani ameongeza kuwa uhusiano wa Iran na majirani zake ni wa kistratijia. Aidha amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina uhusiano mzuri na majirani wote isipokuwa nchi mbili tu ambazo hazitaki kuwa na uhusiano na Tehran.

Rouhani pia ameashiria uwezo mkubwa wa Bandari ya Chahbahar ya kusini mashariki mwa Iran na kuongeza kuwa, inaweza kutumiwa kupitisha mizigo kutoka upande wa kusini hadi kaskazini mwa nchi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu amesema kujengwa reli ya kutoka kusini hadi kaskazini mwa Iran ni mradi wa kimataifa na kuongeza kuwa, reli hiyo itaanzia Bahari ya Hindi katika Bandari ya Chabahar na kuelekea hadi eneo la Asia ya Kati, Caucasia, China, Russia na Ulaya.

Bandari ya Chabahar

Rais Rouhani aidha ameashiria njama za maadui ambao wanataka kuipa Iran pigo na kusema kuweka mashinikizo, kujaribu kuifanya jamii ipoteze matumiani, kuibua mifarakano baina ya wananchi na viongozi, pamoja na kuleta hitilafu baina ya mihimili ya dola nchini Iran ni kati ya malengo ya Marekani na utawala wa Kizayuni.

Rais wa Iran amesisitiza kuwa, wananchi na viongozi wa Iran watashirikiana kusambaratisha njama za maadui.