Onyo la Rouhani kuhusu JCPOA; Ulaya isitumbukie kwenye mtego wa Marekani
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa azimio lilopendekezwa na Marekani katika Barazala Usalama la Umoja wa Mataifa linakiuka moja kwa moja azimio nambari 2231 la baraza hilo na hivyo kuzitaka nchi zote na hasa zilizotia saini mapatano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, zilipinge.
Akizunguza jana Jumatano kwa njia ya simu na Rais mwenzake wa Ufaransa, Emmanuel Macron, Rais Rouhani amesema kwamba Marekani daima imekuwa ikifanya juhudi za kusambaratisha mapatano ya JCPOA na kusisitiza kuwa nchi za Ulaya hazipasi kuhadaika na kunasa kwenye mtego wa nchi hiyo.
Huku muda wa kuondolewa vikwazo vya silaha dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ukikaribia, Marekani inatumia kila mbinu kuhakikisha kuwa vikwazo hivyo vinaendelea kutekelezwa.
Kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa ifikapo tarehe 18 Oktoba mwaka huu na iwapo Marekani itakwenda kinyume na suala hilo basi itakuwa imekiuka azimio hilo. Kwa kujitoa yenyewe kwenye mapatano ya JCPOA, Marekani haina tena haki ya kunufaika na mapatano hayo katika kurudisha vikwazo na kufikia malengo yake mengine ya kisiasa dhidi ya Iran.
Baada ya kufanya mashauriano ya muda mrefu na nchi kadhaa za dunia na hasa za Ulaya, hatimaye Marekani siku ya Jumanne ilisambaza kati ya wanachama wa Baraza la Usalama rasimu ya azimio la kutaka kurejesha vikwazo dhidi ya Iran, suala ambalo halikuungwa mkono na wanachama wengi wa baraza hilo.
Baada ya kuona upinzani huo dhidi yake, Marekani iliamua kufanya marekebisho muhimu katika rasimu ya azimio hilo ili kujaribu kuvutia na kupata ushirikiano wa wanachama wa Baraza la Usalama katika kurefusha vikwazo hivyo vya silaha dhidi ya Iran. Pamoja na hayo lakini bado wanachama muhimu wa baraza hilo wanapinga rasimu hiyo mpya ya Marekani.
Akiashiria suala hilo, Muhammad Jawad Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema Jumatano kwamba; Wamarekani wanatambua vizuri kwamba azimio lao halitapata uungaji mkono katika Baraza la Usalama na baadhi ya tabiri mjini New York zinasema kwamba itafanikiwa kupata kura moja au mbili tu ya wanachama wa baraza hilo.
Wamarekani wamesema kuwa iwapo hawatafikia lengo lao katika Baraza la Usalama, basi watatumia mchakato wa kutatua hitilafu wa JCPOA katika uwanja huo, jambo ambalo halina msingi wowote wa kisheria.
Baada ya kujitoa katika mapatano ya JCPOA, Marekani si mwanachama tena wa mapatano hayo na hivyo haiwezi kuyatumia kufikia malengo yake dhidi ya Iran. Mashinikizo ya Marekani kutumia mchakato huo kwa ajili ya kudhamini maslahi yake ya kisiasa ni hatari dhidi ya mfumo wa fikra na mitazamo kadhaa na kila nchi itakayoamua kushirikiana na nchi hiyo katika hilo itakabiliwa na matokeo mabaya mno.
Katika uwanja huo, Mikhail Ulyanov, mwakilishi wa Russia katika taasisi za kimataifa mjini Vienna Austria alisema siku ya Jumatano kwamba: Juhudi za Marekani kujaribu kurefusha vikwazo vya Iran kwa kutumia mchakato wa kutatua hitilafu wa JCPOA ni chokochoko hatari zinazoweza kusababisha matatizo katika uwanja wa kimataifa.
Msimamo wa Marekani dhidi ya Iran na tishio la kurejesha kwa nguvu vikwazo vya silaha dhidi yake ni mzaha hatari na kejeli dhidi ya michakato ya kimataifa iliyofikiwa kutokana na fikra za pamoja za mataifa na iwapo hilo litatekelezwa ni wazi kuwa hakutakuwepo tena na taasisi yoyote ya kutegemewa na kuaminika katika kudhamini amani na usalama wa dunia.