Zarif: Wanaotumia vibaya mlipuko wa Beirut wanataka kuteteresha amani ya Lebanon
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran leo amekutana na kufanya mazungumzo na Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon mjini Beirut na kusema kuwa, wanaotumia vibaya mlipuko mkubwa uliotokea katika bandari ya Beirut wana nia ya kuyumbisha amani ya Lebanon.
Muhammad Javad Zarif ambaye yuko safarini nchini Lebanon amesema kuwa, wanaotumia vibaya mlipuko wa Beirut ndio wale wale wasiotaka kuwepo utulivu na mshikamano nchini Lebanon.
Sambamba na kuwasilisha salamu za rambirambi za serikali na wananchi wa Iran kwa taifa na serikali ya Lebanon, Zarif amesema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwasaidia watu waliopatwa na maafa katika tukio la bandari ya Beirut na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kushiriki katika ujenzi mpya na ukarabati wa uharibifu na hasara zilizosababishwa na mlipuko wa bandari ya Beirut.
Kwa upande wake Kaimu Waziri Mkuu wa Lebanon, Hassan Diab, ameishukuru Iran kwa misaada yake na kueleza mahitaji ya dharura hususan vifaa vya tiba na zana zinazohitajika kwa ajili ya ukarabati wa nyumba na maeneo yaliyoharibiwa na mlipuko wa Beirut.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran pia amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Lebanon, Nabih Berri na kutangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kushiriki katika operesheni za kukidhi mahitaji ya kipindi kigumu cha sasa ya Lebanon.
Vilevile amelipongeza taifa la Lebanon kwa mnasaba wa kuwadia mwaka wa 14 tangu harakati ya Hizbullah ilipopata ushindi katika vita vya siku 33 vilivyoanzishwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon.