Iran: Marekani haina haki wala kibali cha kutumia "Snapnack Mechanism"
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63155-iran_marekani_haina_haki_wala_kibali_cha_kutumia_snapnack_mechanism
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani haina haki, idhini wala kibali cha kutumia utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN unaofahamika kama 'Snapback Mechanism."
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2020 03:16 UTC
  • Iran: Marekani haina haki wala kibali cha kutumia

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amesema Marekani haina haki, idhini wala kibali cha kutumia utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN unaofahamika kama 'Snapback Mechanism."

Majid Takht-Ravanchi amesema hayo katika hotuba yake kwa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York na kufafanua kuwa, Washington haina haki ya kutumia kipengee cha Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la UN katika hali ambayo, yenyewe ilichukua hatua ya upande mmoja na iliyo kinyume cha sheria ya kujiondoa katika mapatano hayo ya kimataifa.

Amesema Marekani si mwanachama tena wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA baada ya kujitoa kwenye makubaliano hayo mnamo Mei mwaka 2018 na kwa msingi huo, haina haki hata chembe ya kufanya maamuzi juu ya mapatano hayo ya kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo wa Iran amesema Marekani imeanzisha mchakato wa "Snapback Mechanism" baada ya kufeli juhudi zake katika Baraza la Usalama la umoja huo; na hivi sasa imeiweka UN chini ya mashinikizo makubwa ikiwa na hamu ya kuisambaratisha JCPOA.

Baraza la Usalama la UN

Mapema mwezi huu, nchi 13 wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) zilikataa kuiunga mkono Marekani katika njama zake za kutaka kurefushwa vikwazo vya silaha dhidi ya Iran.

Aidha siku chache baadaye, mwenyekiti wa zamu wa baraza hilo alitupilia mbali ombi la US la kutaka kutekelezwa kipengee cha "Snapback Mechanism", ambao ni utaratibu wa kurejesha upya vikwazo ilivyokuwa imewekewa Iran huko nyuma na UN.