UN yatahadharisha kuhusu athari za uharibifu wa mazingira za mlipuko wa Beirut
Umoja wa Mataifa umetahadharisha kuhusu athari mbaya za uhabiribifu wa mazingira za mlipuko uliotoke mwezi uliopita kwenye bandari ya Beirut nchini Lebanon.
Afisa wa mazingira na nishati wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Lebanon amewaambia waandishi habari mjini Geneva kwamba, mbali na idadi ya watu walioaga dunia, mlipuko wa bandari ya Beirut utakuwa na athari nyingine mbaya za muda mrefu kwa mazingira.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema: Japokuwa uchafuzi mkubwa wa mazingira uliotokea baada ya mlipuko huo umepungua lakini chembechembe za kemikali zilizosababishwa na mlipuko huo zinaweza kubakia angani na kuwa na madhara kwa afya ya jamii.
Mlipuko mkubwa uliotokea tarehe 4 Agosti katika bandari ya Beirut ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 190 na kujeruhi wengine karibu 6000. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mlipuko huo umesababisha hasara ya mabilioni ya dola za Marekani.
Nchi nyingi dunia ikiwemo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, zimetuma misada ya hali na mali kwa ajili ya kuwaswaidia watu waliopatwa na madhara kutokana na mlipuko huo.
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran Muhammad Javad Zarif sambamba na kuwasilisha salamu za rambirambi za serikali na wananchi wa Iran kwa taifa na serikali ya Lebanon, alisema Jamhuri ya Kiislamu itaendelea kuwasaidia watu waliopatwa na maafa katika tukio la bandari ya Beirut na kuongeza kuwa, Tehran iko tayari kushiriki katika ujenzi mpya na ukarabati wa uharibifu na hasara zilizosababishwa na mlipuko wa bandari ya Beirut.