Rais Rouhani: Wananchi wa Iran kamwe hawatoipigia magoti Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63287-rais_rouhani_wananchi_wa_iran_kamwe_hawatoipigia_magoti_marekani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia mashinikizo ya kidhalimu ya Marekani dhidi ya Tehran na kusema kuwa, wananchi wa Iran kamwe hawatosalimu amri mbele ya uistikbari wa dola hilo la kibeberu.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 08, 2020 02:39 UTC
  • Rais Rouhani: Wananchi wa Iran kamwe hawatoipigia magoti Marekani

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amegusia mashinikizo ya kidhalimu ya Marekani dhidi ya Tehran na kusema kuwa, wananchi wa Iran kamwe hawatosalimu amri mbele ya uistikbari wa dola hilo la kibeberu.

Rais Hassan Rouhani alisema hayo jana (Jumatatu) wakati alipoonana na Ignazio Cassis, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, kigezo katika uhusiano wa nchi mbalimbali inabidi kiwe ni sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Matiafa. Hata hivyo amesema, kwa miaka mingi Marekani inaendesha njama za kutaka kuipindua Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuingilia masuala ya ndani ya nchi hii ya Kiislamu.

Amesisitiza kuwa, Iran imeheshimu na itaendelea kuheshimu sheria zote za kimataifa na kuongeza kuwa, wakati wowote Marekani itakapokiri kuwa imefanya makosa, basi inaruhusiwa kurejea katika azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uswisi

 

Rais Rouhani amegusia pia baadhi ya jinai za Marekani ikiwa ni pamoja na vikwazo na kuendesha vita vya kiuchumi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitza kuwa, nchi rafiki na huru duniani hazipaswi kunyamazia kimya ugaidi na uvunjaji sheria unaofanywa na Marekani. 

Kwa upande wake, Ignazio Cassis, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uswisi amezungumzia kutimia mwaka wa mia moja tangu kuweko uhusiano wa kisiasa na kidiplomasia baina ya nchi yake na Iran na kusema kuwa, uhusiano wa nchi hizi mbili ni mzuri sana na wa kuheshimia hivyo kuna haja ya kustawishwa na kuimarishwa zaidi uhusiano huo kadiri inavyowezekana.