Iran: Mgogoro wa Afghanistan hauwezi kutatuliwa kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i63416-iran_mgogoro_wa_afghanistan_hauwezi_kutatuliwa_kijeshi
Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna ufumbuzi wa kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Sep 14, 2020 07:58 UTC
  • Iran: Mgogoro wa Afghanistan hauwezi kutatuliwa kijeshi

Mshauri wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hakuna ufumbuzi wa kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan.

Rasoul Mousavi, Mkurugenzi Mkuu wa masuala ya Asia Magharibi katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema mgogoro wa Afghanistan unaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa pekee.

Mousavi amesema hayo leo Jumatatu katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kubainisha kuwa: Naam! Hakuna ufumbuzi wa kijeshi katika mgogoro wa Afghanistan, lakini ieleweke kuwa, ufumbuzi wa kisiasa hautafuata malengo yaliyo sawa na ya kijeshi." Ameongeza kuwa, utatuzi wa kisiasa ni msamaha na mapatano kwa maslahi ya taifa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameashiria kuhusu mazungumzo ya Waafghani yanayofanyika mjini Doha Qatar na kubainisha kuwa, anatumai mkutano huo utapelekea kupatikana amani na uthabiti nchini Afghanistan ili wakimbizi wa Kiafghani popote pale walipo duniani, waweze kurejea nyumbani kwa fahari.

Mazungumzo ya Amani ya Afghanistan mjini Doha

Amesema kuanza mazungumzo ya Doha kuhusu mustakabali wa Afghanistan kumesadifiana na kuanza kwa zoezi la kuwatambua raia wa Afghanistan wanaoishi hapa nchini. Iran ni mwenyeji wa mamilioni ya wakimbizi wa Kiafghani.

Duru ya kwanza ya Mazungumzo ya Waafghani (IAN) iling'oa nanga siku ya Jumamosi mjini Doha kwa kuhudhuriwa na Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, maafisa wa serikali ya Qatar, na wawakilishi wa nchi 30 duniani.