Amir-Abdollahian: Israel inapanga njama ya kuigawanya vipande vipande Saudi Arabia
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amesema: Utawala wa Kizayuni unapanga njama ya kuigawanya vipande vipande Saudi Arabia.
Hossein Amir-Abdollahian ameashiria hatua za utawala wa Kizayuni za kuhakikisha unaanzisha uhusiano wa kawaida na nchi za Kiarabu na kueleza kwamba: Kuanzisha uhusiano wa kawaida na Wazayuni ni usaliti uliofanywa na ufalme wa Abu Dhabi peke yake wala hakukuhusisha falme zingine za Umoja wa Falme za Kiarabu.
Katika ujumbe alioandika kwenye ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Msaidizi maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Katika safari iliyofanywa na mkuu wa shirika la ujasusi la Israel MOSSAD mjini Manama, Bahrain, Aal Khalifa wa Bahrain na Aal-Salman wa Saudia walikuwa si lolote si chochote zaidi ya vibaraka tu wa Marekani na Uingereza na akaongeza kuwa: Israel inakula njama ya kuigawanya vipande vipande Saudi Arabia.
Tangu Donald Trump alipoingia madarakani nchini Marekani, serikali yake imekuwa ikiendesha kampeni ya kuanzishwa uhusiano wa kawaida kati ya nchi za Kiarabu na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel.
Katika utekelezaji wa mpango huo na katika hatua inayopingana na malengo matukufu ya ukombozi wa Palestina, tarehe 15 ya mwezi uliopita wa Septemba mawaziri wa mambo ya nje wa Imarati na Bahrain walisaini makubaliano ya kuutambua rasmi utawala haramu wa Israel na kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na utawala huo unaoikalia Quds tukufu kwa mabavu katika hafla iliyofanyika Ikulu ya White House mjini Washington na kuhudhuriwa na rais wa Marekani Donald Trump.../