Iran yalalamikia uingiliaji wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i6418-iran_yalalamikia_uingiliaji_wa_marekani_katika_ghuba_ya_uajemi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani uingiliaji wa hivi karibuni wa Marekani katika masuala ya usalama wa Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 04, 2016 23:33 UTC
  • Iran yalalamikia uingiliaji wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani uingiliaji wa hivi karibuni wa Marekani katika masuala ya usalama wa Ghuba ya Uajemi.

Katika taarifa, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelalamikia matamshi ya hivi karibuni ya Marekani yaliyo dhidi ya Iran na yenye kuingilia mambo ya ndani ya nchi hii. Aidha Iran imelalamikia vikali hatua ya kutumiwa jina bandia kutaja eneo la maji ya Ghuba ya Uajemi.

Katika taarifa hiyo ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itachukua kila hatua kwa lengo la kulinda usalama na kuhifadhi amani na uthabiti katika Ghuba ya Uajemi."

Taarifa hiyo ya malalamiko ya Iran imekabidhiwa Ubalozi wa Uswisi mjini Tehran ambao unalinda maslahi ya Marekani nchini Iran. Tamko hilo la Iran limetolewa baada ya Randy Forbes, mbunge wa chama cha Republican katika Bunge la Congress nchini Marekani kutaka hatua zichukuliwe kuzuia mazoezi ya kijeshi ya Iran katika Ghuba ya Uajemi.

Siku ya Jumanne, Naibu Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema Iran haitakubali kuwekewa vizingiti na dola lolote duniani katika kutekeleza mazoezi ya kijeshi. Alisistiiza kuwa ni haki ya kisheria ya Iran kufanya mazoezi kwa mujibu wa mipango yake ya kistratijia.