Jeshi la Iran lasema halitaruhusu adui atekeleze hujuma
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa taarifa na kusema liko tayari kukabiliana na tishio lolote lile dhidi ya taifa la Iran na mfumo wa Kiislamu.
Taarifa hiyo imetolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya Tarehe 13 Aban kwa mujibu wa Kalenda ya Kiirani ambayo mwaka huu imesadifiana na Novemba 3. Siku hii ambayo inajulikana kama Siku ya Wanafunzi ni siku ambayo mwaka 1979, wanafunzi Wairani waliteka na kudhibiti pango la ujasusi la Marekani nchini Iran -ubalozi wa Marekani mjini Tehran-, ambalo kwa hakika lilikuwa pigo kubwa la taifa la Iran dhidi ya Marekani.
Katika taarifa hiyo, Jeshi la Iran limesema siku hiyo ni kumbukumbu ya ghadhabu ya taifa la Iran kwa ukatili wa waliokuwa wakiunga mkono utawala ulioangushwa wa kifalme.
Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, historia ya uhasama wa Marekani dhidi ya Iran, hasa baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, inaonyesha kuwa, Marekani daima imekuwa ikilenga kutoa pigo kwa taifa la Iran lakini daima imekuwa ikishindwa. Jeshi la Iran limesema katika taarifa hiyo kwamba, sababu ya kuendelea kushindwa Marekani mkabala wa Iran ni kutokana na kuwa macho taifa la Iran chini ya uongozi wa muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu Amrehemu, na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyed Ali Khamenei.
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limesema miongo minne yenye baraka ya uhai katika Jamhuri ya Kiislamu imeandamana na kufichuliwa uso wa kishetani wa Marekani na uhasama wa shetani huyo na utawala wa Kizayuni dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Hali kadhalika taarifa hiyo imesema stratijia ya mfumo wa Kiislamu wa Iran katika kukabiliana na uistikbari na ukoloni imefaulu na ishara za kuanza kuangamia nguzo za Marekani zinadhihirika wazi.