Vita vya Nagorno-Karabakh kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu
Kuendelea vita vya Armenia na Azerbaijan juu ya eneo la Nagorno-Karabakh kumeibua wasiwasi mkubwa katika eneo hilo.
Akizungumza siku ya Jumanne kupitia televisheni kwa mnasaba wa maulidi ya Mtume Mtukufu (saw) na Imam Swadiq (as), Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa vita hivyo ni tukio chungu ambalo linahatarisha usalama wa eneo na kuongeza kuwa vita hivyo vinapasa kukomeshwa haraka iwezekanavyo. Amesisitiza kuwa ardhi zote za Jamhuri ya Azerbaijan zinazokaliwa na Armenia zinapaswa kuachiliwa na kurejeshewa Azerbaijan.
Kiongozi Muadhamu amesisitiza ulazima wa kulindwa usalama wa Waarmenia wanaoishi katika ardhi hizo na pande mbili kuheshimu mipaka ya kimataifa. Amesema, magaidi ambao kwa mujibu wa ripoti za kuaminika, wameingia katika eneo hilo, hawapasi kuruhusiwa kivyo vyote kukaribia mpaka wa Iran na kwamba iwapo wataukaribia watakabiliwa na jibu kali.
Matamshi ya Kiongozi Muadhamu kuhusu mgogoro wa Karabakh, yanabainisha msimamo wa wazi na wa kimantiki wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu mgogoro unaotonesha donda sugu na kongwe, ambao iwapo hautatafutiwa suluhu ya kudumu unaweza kuchochea ghasia na mivutano zaidi. Katika uwanja huo kuna nukta mbili muhimu ambazo zinapaswa kuangaziwa. Nukta ya kwanza ni tishio ambalo linahatarisha usalama wa eneo iwapo vita vitaruhusiwa kuendelea. Ya pili ni namna ya kutatua mgogoro huo kwa kulindwa ardhi na haki za pande zinazozozana, kwa msingi wa sheria za kimataifa.
Kwa msingi huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran tokea mapigano yaanze kati ya pande mbili katika eneo la Karabakh, imekuwa ikifanya juhudi kubwa kwa madhumuni ya kusimamisha mapigano hayo. Kuhusu suala hilo wiki iliyopita Sayyid Abbas Araqchi, mjumbe maalumu wa Iran katika utatuzi wa mgogoro wa Karabakh alisafiri katika miji mikuu ya nchi za Armenia, Azerbaijan, Russia na Uturuki na kuwasilisha mpango wa Iran kwa ajili ya kuhitimisha mgogoro wa Karabakh. Mjumbe huyo alisema kuwa kukombolewa ardhi za Azerbaijan ni moja ya nukta muhimu za mpango huo na kuongeza kuwa kulindwa haki za binadamu zikiwemo za jamii za wacheche ni suala jingine muhimu linalozingatiwa katika mpango huo unaokusudiwa kumaliza vita vya Karabakh. Mtazamo wa kieneo na kushirikishwa nchi zote husika kieneo katika utatuzi wa mgogoro huo ni nukta nyingine chanya ya mpango huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mgogoro wa Karabakh mwezi Februari 1988 ulibadilika na kuwa vita haribifu ambavyo viliendelea hadi Machi 1994. Hata kama tokea wakati huo pande tofauti zinazojihusisha na mgogoro huo zikiwemo Ulaya na Marekani zimekuwa zikiwasilisha mipango tofauti ya kutatua mgogoro uliopo, ukiwemo mpango wa Minsk, lakini mipango hiyo yote haijakuwa na matokeo ya kuridhisha. Uzoefu unaonyesha kuwa nchi za Magharibi zinafuatilia malengo maalumu katika eneo na kwamba malengo hayo yanadhaminiwa tu kupitia kuchochea moto wa vita na fitina kati ya mataifa ya eneo. Ni wazi kuwa mgogoro wa Armenia na Azerbaijan pia hauko nje ya kanuni hiyo, jambo ambalo bila shaka litakuwa na madhara makubwa kwa maslahi ya kitaifa ya pande mbili zinazozozana na kwa eneo zima kwa ujumla.
Hotuba ya Kiongozi Muadhamu kuhusu matokeo mabaya ya vita vya Karabakh kwa usalama wa eneo ina umuhimu mkubwa kwa mtazamo huo. Katika uwanja huo, Sayyid Abbas Musawi, balozi wa Iran katika Jamhuri ya Azerbaijan ameandika kupitia ujumbe wa Twitter kwamba, kufuatia hotuba hiyo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu mgogoro wa Karabakh, Khalaf Khalafov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Azerbaijan amempigia simu akitoa shukrani za serikali na taifa la Azerbaijan kutokana na hotuba hiyo muhimu na ya kiuadilifu na kusisitiza juu ya kudumishwa urafiki na udugu wa nchi mbili hizi jirani.