Salehi: Marekebisho duniani leo yanahitaji kuhuishwa imani ya dini
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran amesema kuwa, njia pekee ya kuweza kuleta marekebisho ya kweli duniani leo hii ni kuhuishwa imani ya dini katika maana yake ya kina na pana.
Dk Ali Akbar Salehi amesema hayo katika mkutano wa elimu, suluhu, uadilifu, amani na usalama wa kimataifa uliofanyika jana (Jumatano) hapa mjini Tehran na kuongeza kuwa, miongoni mwa changamoto kubwa walizo nazo wanafikra sasa hivi ni suala la kuvunja ubaguzi wa kielimu, kusaidia ufanikishaji wa mchakato wa kuleta suluhu na uadilifu na vile vile kuunga mkono kwa pande zote juhudi za wanaharakati wa masuala ya kijamii kwa ajili ya kulinda mipaka ya amani na usalama wa kimataifa.
Dk Salehi amesema, sasa hivi kuna ushindani usio na huruma wa mababeru wa dunia katika kudhibiti vyanzo vya nguvu, utajiri na nafasi za juu duniani na kubainisha kwamba, wachukuaji maamuzi wa nchi zenye nguvu na baadhi ya wakuu wa ngazi za juu wa maeneo ya kiuchumi na mashirika ya kimataifa wanaziangalia hazina na maliasili za kimaada na kimaanawi za dunia kuwa ni sawa na malighafi ambazo inabidi zitumike kuwanufaisha wao tu.
Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran pia amesema, kutegemea mifumo iliyopo hivi sasa katika uhusiano wa kimataifa kama vile maazimio ya Umoja wa Mataifa, mikataba ya kupiga vita mateso na ya kupambana na uvamizi na ubaguzi hakusaidii chochote. Amesema, wakati umefika kwa walimwengu kurejea kwenye njia ya umaanawi na imani ya dini, kusikiliza na kutekeleza kivitendo ujumbe mkuu waliokuja nao Mitume wa Mwenyezi Mungu.