Iran yaishauri Saudia iache kujipendekeza kwa Israel
Msaidizi maalumu wa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa ameiasa Saudi Arabia ikomeshe mienendo yake ya kujipendekeza, kujidhalilisha na kujikomba kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hossein Amir-Abdollahian ametoa mwito huo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa: Badala ya watawala wa Saudia kujipendekeza na kujitweza mbele ya utawala haramu wa Israel, wanapaswa kuanza kuwaheshimu majirani zao.
Ameeleza bayana kuwa, Mfalme wa Saudia ambaye nchi yake imeivamia Yemen tokea mwaka 2015 na kuisaidia Marekani kuunda genge la kigaidi la Daesh (ISIS) katika nchi za Iraq, Syria, Lebanon na Yemen, hana haki ya kuibua tuhuma dhidi ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran.
Msaidizi Maalumu wa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya kimataifa amebainisha katika ujumbe huo kuwa, Iran daima ndio muungaji mkono mkubwa wa amani na usalama wa majirani zake katika eneo la Asia Magharibi.
Kauli ya afisa huyo wa ngazi za juu wa Iran ni jibu kwa matamamshi ya Mfalme wa Saudia, Salman bin Abdulaziz Aal Saud ambaye juzi Alkhamisi aliitaka dunia eti ichukue msimamo wa pamoja wa kupambana na kile alichokitaja kuwa jitihada za Iran za kuunda silaha za nyuklia na makombora ya balestiki.
Mtawala huyo wa Saudia mwenye umri wa miaka 84 alidai kuwa Iran inaingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, na eti inachochea migawanyiko ya kimadhehebu.