Iran yakanusha madai ya kuzungumza na timu ya Joe Biden
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i64752-iran_yakanusha_madai_ya_kuzungumza_na_timu_ya_joe_biden
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekadhibisha ripoti iliyochapishwa na gazeti la New York Times la Marekani kwamba Tehran imewasiliana na timu ya Rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Nov 20, 2020 23:57 UTC
  • Iran yakanusha madai ya kuzungumza na timu ya Joe Biden

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekadhibisha ripoti iliyochapishwa na gazeti la New York Times la Marekani kwamba Tehran imewasiliana na timu ya Rais mteule wa nchi hiyo, Joe Biden.

Saeed Khatibzadeh amekanusha vikali habari hizo za kipropaganda na kusisitiza kuwa, madai ya New York Times kwamba Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amefanya mawasiliano na timu ya Biden ni ya urongo na yasiyo na msingi wowote.

Akizungumza jana Ijumaa, amesema tayari ofisi ya uwakilishi wa Iran mjini New York imetoa radimali yake kwa habari hizo za upotoshaji na kueleza bayana kuwa, Araqchi hajafanya mazungumzo ya moja kwa moja au yasiyo ya moja kwa moja na maafisa walio karibu na Biden.

Khatibazadeh amesema habari hizo feki ni mfano wa wazi wa 'uanahabari wa manjano' unaotumika sana Marekani kueneza habari za kipropaganda, zisizo na uhakika wala msingi; na zenye vichwa vya kuvutia kwa lengo la kupanua soko la mauzo ya gazeti fulani.

Trump aliiondoa US katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA mwaka 2018

Gazeti la New York Times la Marekani hivi karibuni lilidai kwamba, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi amejaribu kufanya mazungumzo na washauri wa Rais mteule wa Marekani, Joe Biden kupitia wapatanishi.

Hata hivyo Tehran imesisitiza kuwa, Marekani haina budi kurejea katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA pasina masharti yoyote iwapo ina hamu ya kuona mazungumzo yoyote yanafanyika baina ya pande mbili.