Watu 232 wengine wafariki dunia kwa corona nchini Iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 9 wameambukizwa kirusi cha corona na wengine 232 wamefariki dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita.
Daktari Sima Sadat Lari ameeleza hayo leo wakati alipokuwa akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona humu nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu wenye maambukizo, katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 9,594 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 1,408 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.
Aidha Bi Sima Sadam amesema, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia milioni moja na 92,617 na kuongeza, kuwa kutokana na wagonjwa 232 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 51,728.
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa, hadi sasa watu 787,853 wamepata afueni kutokana na maradhi ya Covid-19 humu nchini na wameruhusiwa kurudi nyumbani.
Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, vifo na maambuzi ya corona nchini Iran yameendelea kupungua katika siku za hivi karibuni kufuatia kanuni na sheria kali zinazotekelezwa na serikali ikishirikiana na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Covid-19.
Kimataifa, hadi leo mchana, watu milioni 70 na laki 8 na 35,553 walikuwa wameshaambukizwa corona kote ulimwenguni. Milioni 1 na laki 5 na 91,037 walikuwa wameshafariki dunia na milioni 49 na laki ,2 na 60,905 walikuwa wameshapa afueni. Marekani ndiyo inayoongoza kwa mbali katika maambukizi na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo hatari.