Dec 28, 2020 16:30 UTC
  • Shahidi Qassem Soleimani
    Shahidi Qassem Soleimani

Luteni Jenerali Qassem Soleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alielekea Iraq Januari 3 mwaka 2020 kufuatia mwaliko rasmi wa wakuu wa Iraq.

Punde baada ya kuwasili Iraq aliuawa shahidi katika hujuma ya ndege za kivita za jeshi vamizi na la kigaidi la Marekani karibu na uwanja wa ndege wa Baghdad. Aidha katika hujuma hiyo ya kigaidi Abu Mahdi Al Muhandis, Naibu Mkuu wa Harakati ya Kujitolea ya Wananchi wa Iraq, Abu Mahdi al Muhandi naye pia aliuawa shahidi akiwa ameandamana na Qassem Soleimani. Watu wengine wanane waliokuwa katika msafara huo nao pia waliuawa shahidi.

Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa na nafasi kubwa katika mapambano na maadui pamoja na magaidi na pia katika kuangamiza kundi la kigaidi la Daesh au ISIS. Halikadhalika alikuwa na nafasi muhimu katika kusambaratisha njama ya Marekani na Wazayuni ya kuligawa eneo vipande vipande.

Katika mahojiano ya siku ya Jumapili na Televisheni ya Al Mayadeen, Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah aliashiria nukta hiyo sambamba na kubainisha sifa mbali mbali za shakhsia ya Shahidi Soleimani na alivyokuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha harakati ya muqawama na mapambano ya Kiislamu.

Katibu Mkuu wa Hizbullah katika sehemu ya mahojiano hayo alisema: “Shahidi Soleimani alikuwa mtu wa kwanza aliyetahadharisha kuhusu hatari inayoikabili Syria kwa kisingizo cha mwamko katika nchi za Kiarabu uliojulikana kama " Machipuo ya Kiarabu"kutokana uungaji mkono wa nchi hiyo kwa harakati ya muqawama.”

Katibu Mkuu wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrallah

Sayyid Hassan Nasrallah katika kubainisha umuhimu wa tahadhari hiyo alisema: “Iwapo makundi ya muqawama ya Iraq hayangekuwepo,  hivi sasa kungekuwa na askari 150,000 wa Marekani nchini humo.” Aidha amesema kama si makundi hayo ya muqawama Iraq, leo kinyume cha madai na propaganda za Wamarekani za kutaka demokrasia, leo ubalozi wa Marekani mjini Baghdad ungekuwa ndio unaoiendesha na kuisimamisa Iraq. Aidha amesema kama si makundi ya muqwama ya Iraq, kundi la kigaidi la ISIS lingepata ushindi na kujipenyeza katika eneo zima la Asia Magharibi.

Shahidi Qassem Soleimani kwa hakika alikuwa anafahamu kikamilifu njama za Marekani katika eneo  ambazo zilikuwa zikitekelezwa kwa kutumia bajeti kubwa na idara yenye suhula maalumu na aliweza kuzisambaratisha.

Akizungumza Jumapili mjini Moscow katika Kongamano la Kiislamu  ambalo mada yake kuu ilikuwa, ‘Mkono Mmoja katika Kukabiliana na Changamoto’, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu, Hujjatul Islam Hamid Shahriayari aliashiria nukta hiyo na kuongeza kuwa: “Maadui wa Uislamu waliibua kundi la kigaidi la ISIS ili kwa njia hiyo waweze kuharibu taswira ya Uislamu na Waislamu na hivyo wayafanye mataifa mengine yauogope Uislamu. Aidha kwa kisingizio cha vita dhidi ya ISIS, maadui walilenga kubakisha majeshi yao kinyume cha sheria nchini Syria na Iraq ili kupora utajiri mkubwa wa mafuta na gesi katika eneo la Asia Magharibi.”

Nukta hiyo pia iliashiriwa katika mahojiano ya Sayyid Hassan Nasrallah.

Ushahidi unaonyesha kuwa,  Syria haikulengwa na maadui kwa sababu tu ilikuwa inaunga mkono harakati za mapambano ya Kiislamu au muqawama na wapigania ukombozi wa Palestina. Syria ililengwa pia kwa sababu ina utajiri mkubwa wa mafuta na gesi na pia kutokana na kuwepo kwake katika eneo muhimu kistratijia kwa mtazamo wa kiuchumi, kisiasa na kiusalama.

Ukweli wa mambo ni kuwa, mlingano wa kisiasa na kijeshi umebadilika katika eneo na sasa kuna mwamko miongoni mwa mataifa na serikali na mwamko huo ni wa wanaopinga uingiliaji wa Marekani katika eneo.

Shahidi Abu Mahdi al Muhandis

Jinai ya Marekani katika kumuua Luteni Jenerali Qassem Soleimani na Shahidi Abu Mahdi al Muhandis ni mfano wa wazi wa matokeo ya uwepo wa majeshi ya Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Hivi sasa matukio ya eneo yameingia katika marhala muhimu na yenye kuainisha hatima  ambapo kuna mirengo miwili asili yenye kuainisha hatima hiyo. Katika upande mmoja,  kuna mrengo wa kibeberu ambao unategemea ugaidi na mbinu ya kuzigawa nchi vipande vipande ili kupora utajiri mkubwa wa nchi za Kiislamu sambamba na kuupa nguvu utawala wa Kizayuni unaokalia kwa mabavu Quds Tukufu na Palestina. Katika upande pili kuna harakati ya mwamko wa Kiislamu na muqawama au mapambano ya Kiislamu ambayo lengo lake ni kuvunja njama za maadui ambazo tumezitaja hapo juu. Harakati hii imepata ushindi nchini Syria na imeweza kuthibitisha kuwa ni ya haki. Kuuawa shahidi makamanda wa ngazi za juu katika harakati ya muqawama kama vile Luteni Jenerali Qassem Soleimani ni jambo linalotoadhamana ya kuendelea na kufanikiwa harakati hii ya muqawama katika kukabiliana na njama za adui.

 

Tags