Kamanda wa IRGC: Dei 9 ni siku ambayo Wairani walisimama kupinga fitina
Mratibu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Tarehe Tisa Dei ni siku ya taifa la Iran kwani ni siku ambayo wananchi walijotokeza na kusimama kidete kupinga waliokuwa wameibua fitina.
Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi aliyasema hayo Jumanne mjini Tehran kwa Msikiti wa Lolagar katika hafla iliyofanyika kwa mnasaba wa kukumbuka Hamasa ya 9 Dei.
Itakumbukwa kuwa tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba 2009, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano makubwa kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa machafuko hayo. Machafuko hayo yaliibuliwa na wale waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa rais.
Maandamano ya kupinga machafuko hayo ya fitina yamekuwa tukio muhimu katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi amesema vinara wa fitina hiyo walijinasibisha na Hayati Imam Khomeini, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini pamoja na hayo walitekeleza uharibifu mkubwa.
Ameongeza kuwa, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei ni mtu ambaye alikuwa karibu zaidi na Imam Khomeini na ameyaendeleza Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran bila kukengeuka mkondo wa Imam Khomeini.
Ushahidi na nyaraka zilizopatikana baada ya fitina hiyo zinaonyesha kuwa, vibaraka kutoka nje hususan waliotumwa na Marekani na baadhi ya madola ya Ulaya walikuwa viongozi wa fitina hiyo ya mwaka 2009 ambayo ilizimwa kwa nguvu za wananchi.