Watu wengine 128 waaga dunia kwa Covod-19 nchini Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i65509-watu_wengine_128_waaga_dunia_kwa_covod_19_nchini_iran
Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 6 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 128 wamefariki dunia kwa Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 31, 2020 09:19 UTC
  • Watu wengine 128 waaga dunia kwa Covod-19 nchini Iran

Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran amesema kuwa, watu wengine zaidi ya elfu 6 wameambukizwa virusi vya corona na wengine 128 wamefariki dunia kwa Covid-19 katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Bi Sima Sadat Lari amesema hayo leo wakati akitoa takwimu za karibuni kabisa za maambukizi ya corona hapa nchini na kuongeza kwamba, kwa mujibu wa matokeo ya vipimo rasmi walivyofanyiwa watu  katika muda wa masaa 24 yaliyopita wagonjwa wapya 6,390 waliokumbwa na ugonjwa wa COVID-19 wamegunduliwa humu nchini, ambapo 702 miongoni mwao wamelazwa hospitalini na waliobakia wamepatiwa huduma za tiba na kurudi nyumbani.

Kadhalika  Dakta Lari  amesema kuwa, idadi ya watu waliogunduliwa kupatwa na ugonjwa wa COVID-19 nchini Iran hadi hivi sasa imefikia 1,225,143 na kuongeza kuwa kufuatia wagonjwa 128 kuaga dunia katika kipindi cha masaa 24 yaliyopita, jumla ya watu waliofariki dunia hadi sasa hapa nchini kutokana na ugonjwa huo imefikia 55,223.

Mwanadamu wa kwanza kujitolea kudungwa chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa Iran inayojulikana kama COVIRAN Barekat akidungwa chanjo hiyo katika uzinduzi uliofanyika Tehran Disemba 29, 2020

 

Msemaji wa Wizara ya Afya, Tiba na Mafunzo ya Utabibu ya Iran ameongeza kuwa hadi sasa watu 988,838 wamepona maradhi ya Covid-19 hapa nchini na kuruhusiwa kurudi nyumbani. 

Wakati huo huo, Naibu Waziri wa Afya na Mafunzo ya Tiba wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hadi hivi sasa hakuna athari zozote hasi zilizooneshwa na watu waliofanyiwa majaribio ya chanjo ya corona, licha ya kupita zaidi ya masaa 24 ya tangu kudungwa chanjo hiyo.

Mwanadamu wa kwanza kabisa kufanyiwa majaribio ya chanjo ya COVID-19 iliyotengenezwa na Iran na ambayo inajulikana kwa jina la kiutaalamu la "Coviran Barekat" alifanyiwa majaribio hayo juzi Jumanne.