Iran yafanya mazoezi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran linafanya mazoezi makubwa zaidi ya ndege zisizo na rubani au drone.
Jana Admirali Sayyid Mahmoud Mousavi, naibu wa operesheni wa mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu alisema kuwa, mazoezi hayo makubwa ya kijeshi ya ndege zisizo na rubani za Iran yanafanyika katika mazingira halisi ya kivita yakishirikisha vikosi vya nchi kavu, vikosi vya ulinzi wa anga na rada, vikosi vya majini na angani vya Jeshi la Iran na inabidi droni hizo ziendeshe operesheni zake kwa njia bora kabisa.
Wakati huo huo, akizungumza pembizoni mwa mazoezi hayo, Mkuu wa Kamandi ya Majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Meja Jenerali Mohammad Baqeri amesema majeshi ya Iran yako tayari kabisa kukabiliana na kosa lolote litakalofanywa na adui.
Amesema ingawa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina nia ya kuanzisha vita au hujuma dhidi ya nchi yoyote jirani, lakini iko tayari kukabiliana na tishio lolote lile.
Kauli hiyo imekuja baada ya Waziri wa Ulinzi wa Marekani Christopehr Miller kuamuru meli ya kivita ya Marekani yenye kusheheni ndege, USS Nimitz, ibakie katika Ghuba ya Uajemi kutokana na kile alichodai kuwa ni tishio la Iran dhidi ya rais Trump na maafisa wengine wa Marekani.