Watu 2 wauawa katika tukio la utekaji nyara jimboni Texas, Marekani
Watekajinyara wamewaua watu wawili katika jimbo la Texas, Marekani.
Gazeti la Daily Mail limeripoti kuwa, polisi ya mji wa Austin jimboni Texas jana usiku ilitangaza kuwa, tukio hilo la utekaji nyara lilijiri kwa muda wa saa sita katika kituo kimoja cha tiba cha watoto katikati mwa mji huo. Imesema kuwa, miili ya watu wawili imekutwa ndani ya kituo hicho cha tiba.
Polisi ya mji wa Austin imeongeza kuwa, mtu mmoja aliyekuwa na silaha aliingia katika kituo hicho cha tiba cha watoto katikati ya mji huo na kuteka nyara idadi ya watu isiyojulikana. Kwa kuzingatia kuwa, tukio hilo la utekaji nyara limemalizika lakini wahusika wake bado hawajatambuliwa hadi sasa.
Kitendo cha kuwa huru ubebaji silaha huko Marekani kimepelekea kushuhudiwa vitendo vya utumiaji mabavu na machafuko nchini humo. Aidha kila mwaka maelfu ya watu huuliwa na kujeruhiwa kwa kupigwa risasi katika maeneo mbalimbali nchini Marekani.
Lobi ya silaha nchini humo ina nguvu kubwa kiasi kwamba Kongresi ya Marekani pia imeshindwa kuchukua hatua za kuzuia ubebaji silaha kiholela nchini humo. Ripoti rasmi zinaeleza kuwa, kuna karibu silaha moto milioni 270 hadi 300 huko Marekani; yaani takribani kila mtu mmoja ana bunduki moja nchini humo.