Vaezi: Israel haina nguvu za kijeshi za kutoa pigo kwa Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66176-vaezi_israel_haina_nguvu_za_kijeshi_za_kutoa_pigo_kwa_iran
Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel hauna mpango, uwezo, nguvu wala mkakati wa kulishambulia kijeshi taifa hili.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 28, 2021 00:47 UTC
  • Vaezi: Israel haina nguvu za kijeshi za kutoa pigo kwa Iran

Mkuu wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema utawala wa Kizayuni wa Israel hauna mpango, uwezo, nguvu wala mkakati wa kulishambulia kijeshi taifa hili.

Mahmoud Vaezi alisema hayo jana Jumatano pambizoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri na kueleza bayana kuwa, vikosi vya majeshi ya Iran likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) vimepewa mafunzo ya hali ya juu ya kulihami taifa hili.

Ameashiria matamshi ya hivi karibuni ya Mkuu wa Majeshi ya Israel aliyedai kuwa utawala huo umepanga kuishambulia kijeshi Iran ambapo amesisitiza kuwa, "wananchi wa Iran na wa eneo hili (la Asia Magharibi) kwa ujumla wamezoea bwabwaja za aina hiyo za maafisa wa Israel."

Vaezi amebainisha kuwa, lengo la utawala haramu wa Israel kuropoka na kutoa matamshi hayo ya kipropaganda ni kuendeleza vita vyake vya kisaikolojia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Mkuu wa Ofisi ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, majeshi ya Iran hayana azma ya kuanzisha vita dhidi ya yeyote, lakini yamejiandaa vya kutosha kujibu chokochoko za maadui.

Baadhi ya makombora ya Iran

Kadhalika amesema utawala wa Kizayuni na baadhi ya nchi katika eneo hili ikiwemo Saudi Arabia hazitaki kabisa kusikia suala la Marekani kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA na kuliondolea taifa hili vikwazo vya kidhalimu.

Mkuu wa majeshi ya Israel amemtaka Rais mpya wa Marekani Joe Biden asiirejeshe Washington katika makubliano hayo ya kimataifa, ambapo ametishia kuwa, iwapo atafanya hivyo basi utawala huo utatafakari hatua za kijeshi za kuchukua dhidi ya Iran.