AEIO yasema Iran itazindua miradi 50 ya nyuklia karibuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i66674-aeio_yasema_iran_itazindua_miradi_50_ya_nyuklia_karibuni
Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu itazindua miradi 50 ya mafanikio ya sekta ya nyuklia ya taifa hili karibuni hivi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 09, 2021 23:00 UTC
  • AEIO yasema Iran itazindua miradi 50 ya nyuklia karibuni

Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran (AEOI) amesema Jamhuri ya Kiislamu itazindua miradi 50 ya mafanikio ya sekta ya nyuklia ya taifa hili karibuni hivi.

Ali Akbar Salehi alisema hayo jana Jumanne pambizoni mwa sherehe za ufunguzi wa Maonyesho ya Kudumu ya Mafanikio ya Sekta ya Nyuklia huko Qazvin, kaskazini magharibi mwa Tehran na kuongeza kuwa, uzinduzi wa miradi hiyo utafanyika Aprili 9, itakayosadifiana na Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia hapa nchini. 

Dakta Salehi ameeleza bayana kuwa, wataalamu na wanasayansi katika taasisi ya AEOI wamefanya jitihada kubwa za kuistawisha sekta ya nyuklia ya Iran, na natija ya juhudi hizo zitaanza kuonekana karibuni hivi.

Amesema wataalamu na maafisa wa sekta ya nyuklia walionyesha utayarifu wa hali ya juu hivi karibuni, wakati ambapo Jamhuri ya Kiislamu iliamua kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20, ambapo kazi hiyo kubwa ilifanyika ndani ya saa 12 pekee.

Iran inasisitiza kuwa miradi yake ya nyuklia ni kwa malengo ya amani

Mkuu wa Taasisi ya Atomiki ya Iran ameongeza kuwa, hivi sasa katika utendaji kazi wa taasisi ya AEOI ya Iran, muda uliopo baina ya wazo kuwasilishwa, kutathminiwa, kufanyiwa kazi na hata kuzalishwa huwa mfupi mno, na wataalamu wa nyuklia wa Iran wametabahari katika kulisukuma mbele gurudumu la sekta hiyo kwa umakinifu mkubwa na kwa muda mfupi.

Tarehe 9 Aprili, Iran itaadhimisha Siku ya Kitaifa ya Teknolojia ya Nyuklia, maadhimisho ambayo hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwashukuru na kuwaenzi wanasayansi Wairani wa nyuklia ambao wameiletea nchi hii fahari na kuiwezesha kukamilisha mzunguko kamili wa kutengeneza fueli ya nyuklia.