Rouhani: Haiyumkiniki kujumuisha maudhui nyingine katika JCPOA
(last modified Thu, 18 Feb 2021 03:14:20 GMT )
Feb 18, 2021 03:14 UTC
  • Rouhani: Haiyumkiniki kujumuisha maudhui nyingine katika JCPOA

Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema ni jambo lisilowezekana kuarifisha na kujumuisha maudhui nyinginezo katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika mazungumzo yake ya simu na Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani jana Jumatano, Rais Rouhani alizikosoa nchi za Ulaya kwa kufeli kutekeleza majukumu yao ndani ya JCPOA baada ya Marekani kujiondoa katika mapatano hayo.

Ameeleza bayana kuwa, "JCPOA ina fremu maalumu isiyobadilishika, na iwapo Ulaya inataka kuyalinda mapatano hayo kikweli, lazima idhihirishe hilo kivitendo." Baadhi ya nchi za Ulaya zinataka kujumuishwa uwezo wa makombora wa Iran na ushawishi wa taifa hili katika eneo la Asia Magharibi kwenye mapatano hayo ya kimataifa, miito ambayo Tehran imeyapuuzilia mbali.

Dakta Rouhani amesisitiza kuwa, Marekani itakapoiondolea Iran vikwazo haramu na kurejea katika Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, basi Jamhuri ya Kiislamu itarejea mara moja katika utekelezaji wa wajibu wake katika mapatano hayo.

Amesisitiza kuwa, serikali ya Tehran ina jukumu la kupunguza uwajibikaji wake ndani ya mapatano hayo kwa mujibu wa sheria iliyopasishwa na Bunge la Iran na kwamba kwenda kinyume na hayo, ni kukanyaga sheria za nchi.

Vikwazo haramu na vya kidhalimu vya US dhidi ya taifa la Iran

Kadhalika Rais Rouhani katika mazungumzo yake ya simu na Kansela wa Ujerumani ametoa mwito wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili wa Iran na Ujerumani katika nyuga mbalimbali hususan kuimarishwa ushirikiano wa makampuni na sekta binafsi za nchi mbili hizi.

Kwa upande wake, Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani amesisitizia udharura wa kuilinda JCPOA kama mapatano ya kimataifa, huku akitoa mwito wa kupatia ufumbuzi tofauti zilizopo kupitia njia za mazungumzo. Amesema kuimarishwa uhusiano na ushirikiano wa pande zote husika ni kwa maslahi ya usalama na uthabiti wa eneo zima.

Tags