Rais Rouhani: Mapatano ya JCPOA hayalindiki kwa kaulimbiu na maneno, yanahitaji vitendo
(last modified Wed, 03 Mar 2021 13:50:43 GMT )
Mar 03, 2021 13:50 UTC
  • Rais Rouhani: Mapatano ya JCPOA hayalindiki kwa kaulimbiu na maneno, yanahitaji vitendo

Rais Hassan Rouhani amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasubiri kuona hatua za kivitendo kuhusiana na makubaliano ya nyuklia na akasisitiza kuwa makubaliano hayo ya JCPOA hayalindiki kwa kaulimbiu na maneno matupu.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyasema hayo leo katika kikao cha Baraza la Mawaziri ambapo sambamba na kuashiria kuwa serikali ya sasa ya Marekani imekiri kuhusu mwenendo ghalati na potofu wa serikali iliyotangulia, ameongeza kwamba, kwa upande wa Iran jambo la msingi na muhimu zaidi ni kuondolewa vikwazo na kupatikana haki za wananchi wa Iran, hata hivyo hakuna hatua ya maana iliyochukuliwa na upande wa serikali ya Marekani.

Rais Rouhani amesema, ikiwa Marekani itaondoa vikwazo vyote, Iran nayo itatekeleza papo hapo ahadi na majukumu yake yote na akabainisha kuwa, Marekani na Ulaya zinatoa kaulimbiu na kusema 'tunataka kurudi kwenye JCPOA'; lakini kaulimbiu tupu hazitoshi, bali inapasa zichukue hatua kivitendo.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameashiria pia ushawishi wa Wazayuni kwa uchukuaji maamuzi wa rais aliyetangulia wa Marekani Donald Trump na akasema: Yeye pia alikuwa kidhahiri akitoa kaulimbiu kwa kusema Marekani Kwanza, lakini katika uchukuaji hatua, Uzayuni ndio uliokuwa wa kwanza, wa pili ikawa ni msimamo ya kufurutu mpaka, wa tatu ukawa ni ubaguzi wa rangi na Marekani ikawa ya nne. Rais Rouhani ameongeza kuwa, Wazayuni walimghilibu Trump na kumuongoza kwenye njia potofu.../

Tags