Arab League yatakiwa iache kutoa taarifa zisizo na msingi
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameitaka Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ijiepushe na tabia yake ya kutoa taarifa zisizo na msingi wowote na badala yake, ikumbatie mambo ambayo yanaweza kuimarisha ushirikiano wa nchi za eneo.
Kauli ya Saeed Khatibzadeh ni radiamali kwa tangazo la hivi karibu la Kamati ya Pande Nne ya Arab League, lililokuwa limesheheni madai yasiyo na msingi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Khatibzadeh ameeleza bayana kuwa, 'inasikitisha kuona nchi fulani za Kiarabu zinapotosha fikra za walio wengi, kwa kujaribu kuficha nyendo zao haribifu na ghalati, badala ya kupatia ufumbuzi matatizo halisi yanayoukabili ulimwengu wa Kiarabu."
Saeed Khatibzadeh amebainisha kuwa, mataifa ambayo kwa miaka sita sasa yameivamia Yemen na kuharibu kikamilifu miundomsingi ya nchi hiyo, na kuwasababishia Wayemen baa la njaa, magonjwa, umaskini na kuwafanya mamilioni miongoni mwa wawe wakimbizi, huku damu za watu wasio na hatia zikitapaka katika mikono yao, sasa yanajaribu kujiondolewa lawama kwa kuibua tuhuma zisizo na msingi.

Wakati huohuo, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amepuuzilia mbali madai yasiyo na maana ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu juu ya visiwa vitatu vya Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kuwa, visiwa hivyo ni sehemu isiyotenganishika na ardhi ya Iran.
Amefafanua kuwa, azimio la Arab League kuwa Jamhuri ya Kiislamu imekaliwa kwa mabavu visiwa vitatu vya Tunb Kubwa, Tunb Ndogo na Abu Musa vya vya kusini mwa Iran eti vya Imarati katika Ghuba ya Uajemi haliwezi kubadilisha ukweli wa kihistoria na kijiografia juu ya maeneo hayo.