Rouhani: Iran inalipa kipaumbele suala la Usalama na amani Iraq
Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi na kusisitiza kuwa, usalama, mshikamano na amani Iraq ni kipaumbele muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Rais Rouhani ameyasema hayo Jumamosi katika mazungumzo ya simu na Waziri Mkuu wa Iraq Mustafa al Kadhimi na kuongeza kuwa, Iran inapinga uingiliaji wowote wa kigeni katika masuala ya ndani ya Iraq kwani jambo hilo si tu kuwa ni kwa madhara ya Iraq bali pia kwa eneo zima.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, kuimarishwa kiwango cha uhusiano wa kiuchumi sambamba na uhusiano wa kisiasa ni nukta yenye umuhimu mkubwa. Aidha ametaka yarahisishwe masuala ya utoaji visa kwa ajili ya wafanyabiashara na pia kuandaliwe mazingira mazuri ya wawekezaji wa sekta binafsi ili kuimarisha zaidi uhusiano wa Iran na Iraq.
Rais wa Iran aidha ameashiria kuwa, hivi sasa mabilioni ya dola za Iran zimekwamishwa kinyume cha sheria katika benki za Iraq pamoja na kuwa viongozi wa nchi hiyo wametoa ahadi mara kadhaa ya kuachilia fedha hizo. Amesema kuna udharura wa fedha hizo kukabidhiwa Iran haraka iwezekanavyo.
Rais Rouhani ameongeza kuwa, daima Wamarekani wamekuwa na nafasi haribifu katika eneo, na hivyo kutekelezwa haraka agizo la Bunge la Iraq kuhusu kuondoka wanajeshi wa Marekani nchini humo kunaweza kurejesha utulivu katika eneo.
Kwa upande wake Waziri Mkuu wa Iraq amesema Iran ni nchi rafiki na jirani na kuongeza kuwa, kuunganisha reli za nchi mbili ni hatua muhimu katika ustawi wa uhusiano wa kiuchumi wa na kibiashara baina ya Tehran na Baghdad.
Al Kadhimi pia ameishukuru Iran kwa kuisaidia Iraq katika kurejesha usalama na uthabiti nchini humo na kuongeza kuwa, vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran ni vya kidhalimu na kinyume cha sheria.