Iran kuwaanika wahusika wa shambulio dhidi ya meli yake ya mizigo
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu inafuatilia suala la kuwatambua watu waliohusika na shambulio la kigaidi dhidi ya meli ya mafuta ya nchi hii katika maji ya kimataifa na karibuni hivi itawaanika.
Sambamba na kulaani shambulio hilo, Saeed Khatibzadeh amesema: Vyombo husika vya Iran vinafuatilia kwa karibu hujuma hiyo iliyokiuka sheria za kimataifa na sheria za ubaharia, na karibuni itawatambua waliohusika na shambulio hilo.
Ameeleza bayana kuwa, kuwatambua waliohusika na jinai hiyo ya siku chache zilizopita katika Bahari ya Mediterrania ni katika ajenda kuu ya vyombo mbalimbali vya Iran.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameongeza kuwa, shambulio hilo la kigaidi dhidi ya meli ya mizigo ya Iran tena katika maji ya kimataifa ni mfano wa wazi wa ukanyagaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na maadui wa taifa hili.

Ali Ghiasian, Msemaji wa Shirika la Usafiri wa Baharini la Iran siku ya Ijumaa alisema, meli hiyo ya mizigo ya Iran ya Shahr-e Kord ilishambuliwa kwa mada za miripuko siku ya Jumatano katika Bahari ya Mediterrania, lakini hakuna baharia aliyeuawa au kujeruhiwa vibaya kwenye tukio hilo la kigaidi.
Ameongeza kuwa, moto uliosababishwa na mripuko huo ulizimwa haraka na mabaharia waliokuweko katika meli hiyo ya Iran na kisha ikaendelea na safari yake.