Iran yatoa mkono wa pole kwa Tanzania kufuatia kifo cha Rais Magufuli
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma salamu za mkono wa pole kwa wananchi na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia kifo cha rais wa nchi hiyo John Pombe Magufuli.
Saeed Khatibzadeh ameeleza masikitiko ya wananchi na serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa wananchi na serikali ya Tanzania kwa kifo cha kiongozi wa nchi hiyo.
Rais John Magufuli alifariki dunia siku ya Jumatano kwa matatizo ya moyo katika Hospitali ya Mzena mjini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.
Rais Magufuli aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 61, aliingia madarakani mwaka 2015. Alichaguliwa tena kwa muhula wa pili katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 2020.
Viongozi wa nchi na mataifa mbali mbali duniani wametuma salamu za rambirambi kwa serikali na wananchi wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais Magufuli.
Kufuatia kifo cha kiongozi huyo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan jana Ijumaa, aliapishwa kuwa rais mpya wa nchi hiyo.
Samia, ambaye ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya Tanzania na katika eneo la Afrika Mashariki, amewaomba wananchi kushikamana katika kipindi hiki na kwamba wasiwe na hofu kwani nchi hiyo inayo hazina nzuri ya viongozi wakiwemo waliostaafu, hivyo hakuna jambo litakaloharibika.
Tangu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoundwa mwaka 1964, hayati John Magufuli ni rais wa kwanza kufariki dunia akiwa angali yuko madarakani.../