Iran: Hatujapokea ujumbe wowote kutoka Marekani
(last modified Sat, 20 Mar 2021 08:19:18 GMT )
Mar 20, 2021 08:19 UTC
  • Iran: Hatujapokea ujumbe wowote kutoka Marekani

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema Jamhuri ya Kiislamu haijapokea ujumbe wowote kutoka kwa Marekani wala haina azma yoyote ya kuitumia Washington ujumbe.

Saeid Khatibzadeh amesema hayo leo Jumamosi katika mahojiano maalumu na shirika la habari la Sputnik la Russia na kuongeza kuwa, kinachopaswa kufanyika hivi sasa ni kwa Marekani kuliondolea taifa hili vikwazo vya kidhalimu.

Amesema Marekani inapaswa kufungamana na majukumu na ahadi zake, irejee katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na iiondolee Iran vikwazo ambavyo vimeisababishia Jamhuri ya Kiislamu hasara ya dola trilioni moja.

Khatibzadeh ameeleza bayana kuwa: Hadi sasa hatujapokea ujumbe wowote kutoka utawala mpya wa Marekani ama kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja.

Bendera za nchi washiriki wa JCPOA

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, JCPOA ina ramani ya njia ya kutatua mzozo uliopo na kwa msingi huo hakuna mazungumzo yanayohitajika kwa ajili ya pande husika kurejea katika mapatano hayo, wala pande husika hazipaswi kutumiana jumbe juu ya kadhia hiyo.

Amesisitiza kuwa, sera ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya Washington dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefeli kwa kuwa uchumi wa taifa hili unaendelea kustawi licha ya mashininikizo na vikwazo hivyo.

 

 

 

Tags