Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu JCPOA; Iran haina haraka
(last modified Tue, 23 Mar 2021 09:45:50 GMT )
Mar 23, 2021 09:45 UTC
  • Mtazamo wa Kiongozi Muadhamu kuhusu JCPOA; Iran haina haraka

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, Marekani inapaswa kufuta vikwazo vyote, kisha Iran ichunguze na kutathmini ukweli wa hatua hiyo, na endapo itathibiti kweli kwamba, vikwazo hivyo vimeondolewa, basi taifa hili litarejea bila tatizo lolote katika utekelezaji wa ahadi zake kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo katika hotuba yake kwa mnasaba wa mwaka mpya wa Hijria Shamsia wa 1400 na kubainisha kwamba, ahadi za Wamarekani si za kuaminika hata watu waamini kuondolewa vikwazo katika makaratasi, bali vikwazo hivyo vinapaswa kuondolewa katika medani ya vitendo na kisha Jamhuri ya kiislamu kutathmini ukweli wa hatua hiyo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kuwa, baadhi ya Wamarekani wanaamini kuwa, mazingira ya sasa yana tofauti na kile kipindi ambacho makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yalitiwa saini, na hivyo JCPOA nayo inapasa kubadilishwa.

Ndio, bila shaka mazingira yamebadilika na hivi sasa ni kwa madhara ya Marekani, na kama itakuwa kwamba, makuabliano haya yabadilishwe basi yanapasa kubadilishwa kwa maslahi ya Iran.

 

Baada ya kupita miezi miwili tangu kushika hatamu za uongozi Joe Biden nchini Marekani, siasa za Washington kuhusiana na Iran na hata makubaliano ya JCPOA zipo katika mkondo ule ule wa miaka mine iliyopita; mkondo ambao Donald Trump akitumia “siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa” alifanya hima ya kuivuta tena Iran katika meza ya mazungumzo ili apate fursa ya kuongezea vitu vipya katika makubaliano hayo.

Misimamo ya hivi karibuni ya timu ya sera za kigeni ya Rais Joe Biden wa Marekani inaonyesha kuwa, Wamarekani wakitumia mashinikizo na dipolmasia ya mabavu, wanafuatilia suala la kupata upendeleo mpya kutoka kwa Iran na kuongeza mambo mapya katika orodha ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA. Tajiriba ya miaka minne ya siasa za Trump mkabala na Iran ambazo zilishindwa na kugonga mwamba, hivi sasa ipo mbele ya Joe Biden na bila shaka kupita katika njia hiyo hiyo aliyopitia Trump hakuwezi kulifanya taifa shupavu la Iran lisalimu amri.

Kama alivyositiza Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hotuba yake ya Nairuz (mwaka mpya wa Hijria Shamsia) ni kuwa, mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa yameshindwa na kugonga ukuta; na kama serikali mpya ya Marekani itataka kufuata siasa na sera hizo hizo, yenyewe pia itashindwa na badala yake Iran itazidi kuwa imara siku baada ya siku.

Rais Joe Biden wa Marekani

 

Siasa madhubuti za Iran kuhusu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA zimetangazwa wazi na bayana na kama zitakubaliwa hapana shaka kuwa, hali ya mambo itabadilika. Lakini kama pande zingine katika makubaliano hayo hususan Marekani zitakataa, hali ya sasa itaendelea na Iran haina haraka kuhusiana na suala la kuondolewa vikwazo na kurejea Washington katika makubaliano hayo.

Wamarekani ili warejee katika JCPOA na kuondoa vikwazo wamekuwa wakizungumzia suala la nani anapaswa kuchukua hatua ya kwanza, maneno ambayo kwa hakika hayana nafasi kabisa. Hii ni sababu, suala la msingi lililokuwa likizungumziwa ni utekelezaji wa ahadi kwa mujibu wa makubaliano ya JCPOA na Marekani ndio iliyokiuka makubaliano hayo, hivyo yenyewe ndiyo inayopaswa kutekeleza kivitendo ahadi ilizotoa kwa mujibu wa makubaliano hayo.

Iran baada ya kutia saini makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ilitekeleza ahadi zake, lakini pande zingine katika makubaliano hayo zilikiuka ahadi zao.

 

Katika mazingira kama haya, hii leo haiwezekani hata kidogo kuamini ahadi na maneno yao. Kwa mujibu wa JCPOA, Iran ilipunguza baadhi shughuli zake kama urutubishaji wa madini ya Urani, lakini la kusikitisha ni kuwa, pande nyingine hazijaweza kudhamini maslahi ya kiuchumi ya taifa hili katika fremu ya makubaliano hayo.

Baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na Ulaya na pande zingine katika makubaliano hayo kushindwa kudhamini maslahi ya kiuchumi ya Iran kama ilivyokuwa imekubaliwa, taifa hili lilichukua hatua ya kupunguza ahadi zake kwa awamu na hii leo urutubishaji wa madini ya Urani wa asilimia 20 unafanyika hapa nchini.

Anga inayotawala hivi sasa katika kadhia ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA inadhihirisha umakini na nguvu ya Iran na taifa hili limeendelea kusukuma mbele gurudumu la miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani kwa usimamizi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA). Aidha katika njia ya kuhuisha makubaliano ya JCPOA, Iran haipotezi fursa na wala haina haraka katika hili, bali inachokifikiria na kukizingatia ni maslahi na manufaa yake ya kisheria.

Tags