Ajenda ya kikao cha JCPOA Vienna itakuwa ya kujadili masuala ya kisheria
Afisa mmoja husika katika ujumbe unaoiwakilisha Iran katika kikao cha kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kitakachofanyika kesho mjini Vienna amesema, ajenda ya mazungumzo ya kamati hiyo itahusu majadiliano juu ya masuala ya kisheria tu kuhusu namna pande mbili zitakavyotekeleza majukumu yao na kupatikana uthibitisho wa utekelezaji huo.
Kauli hiyo imekuja baada ya kutolewa taarifa kadhaa na maafisa wa nchi za Magharibi kuhusu kujumuishwa kwenye mazungumzo hayo mipango ya makombora na ya kikanda ya Iran, wakati sharti la Iran la kurudi kwenye utekelezaji kamili wa JCPOA ni kuondolewa kikamilifu na kwa mpigo vikwazo ilivyowekewa na Marekani na kisha kupata hakikisho la taathira chanya za hatua hiyo; na si uondolewaji wa hatua kwa hatua.
Kwa mujibu wa afisa huyo, ikiwa nchi zinazounda kundi la 4+1 zitaweza kuishawishi Marekani ikubali kufanya hivyo, ndipo Iran itarudi kwenye utekelezaji wa majukumu yake katika makubaliano ya nyuklia, vyenginevyo Tehran itaendelea na msimamo inaofuata hivi sasa bila ya kuwa na papara ya kuchukua hatua yoyote.

Hapo kabla, Sayyid Abbas Araqchi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa alishasisitiza, "kuhusu pande zote kurudi kwenye utekelezaji wa JCPOA, tutafanya mazungumzo na kundi la 4+1 tu na hatutakuwa na mazungumzo yoyote ya ana kwa ana au yasiyo ya ana kwa ana na Marekani; na katika kikao hiki tutabainisha misingi inayoendana na sera zilizotangazwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi."
Kikao cha msimu cha kamati ya pamoja ya makubaliano ya nyuklia ya JCPOA kinafanyika kesho mjini Vienna kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa Iran na wa nchi zinazounda kundi la 4+1.../