Raisi: Shahidi Soleimani, chimbuko la ushindi mkabala wa maadui
(last modified Tue, 04 May 2021 01:34:20 GMT )
May 04, 2021 01:34 UTC
  • Raisi: Shahidi Soleimani, chimbuko la ushindi mkabala wa maadui

Mkuu wa Vyombo vya Mahakama vya Iran amesema Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) alikuwa chanzo cha ushindi mtawalia dhidi ya maadui.

Ayatullah Sayyid Ibrahim Raisi alisema hayo jana Jumatatu katika mkutano wa kila wiki wa Baraza Kuu la Idara ya Mahakama ya Iran na kuongeza kuwa, "Luteni Jenerali Qassem Soleimani alikuwa kamanda, shakhsia na mtu aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika ulimwengu wa Kiislamu.

Raisi ameeleza bayana kuwa, Shahidi Soleimani ameacha athari kubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, na umma huo daima utamkumbuka kwa kuwa chimbuko la uthabiti na ushindi mtawalia dhidi ya maadui katika mataifa ya Kiislamu.

Ikumbukwe kuwa, Februari mwaka huu, Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliutembelea mji mkuu wa Iraq, Baghdad na kuzuru eneo walipouawa shahidi kamanda Qassem Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis na kutoa heshima zake kwa mashahidi hao wawili.

Mashahidi Soleimani na Abu Mahdi al Muhandis

Alisisitiza kuwa,  jinai iliyofanywa na Marekani ya mauaji ya makamanda hao wa muqawama haitaachwa bila ya jibu na akabainisha kuwa, shahidi Qassem Soleimani na shahidi Abu Mahdi al Muhandis ni mashujaa wa mapambano dhidi ya ugaidi.

Wawili hao pamoja na wenzao wanane waliuawa shahidi mnamo Januari 3 mwaka 2020 katika shambulio la anga lililofanywa na wanajeshi magaidi wa Marekani, kwa amri ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo ya kibeberu Donald Trump.