Jenerali Salami: Pigo la kwanza kwa Israel, yumkini likawa la mwisho
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran (IRGC) amesema wimbi la migogoro ya kiusalama lililoshuhudiwa katika siku za hivi karibuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) limeonesha wazi udhaifu na hatari inayoukabili utawala wa Kizayuni wa Israel.
Brigedia Jenerali Hossein Salami amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la IRIB usiku wa kuamkia leo na kueleza bayana kuwa, povu la usalama wa Israel limeshapasuka na hivi sasa taswira halisi ya utawala huo imedhihiri machoni pa walimwengu.
Brigedia Jenerali Salami amesema picha ambayo utawala huo khabithi umekuwa ukiionesha dunia kupitia propaganda na operesheni zake za kisaikolojia imeshachanika.
Amebainisha kuwa, matukio kadhaa yaliyoshuhudiwa katika kipindi cha mwezi mmoja hadi miwili iliyopita ndani ya utawala huo haramu yanaonesha udhaifu wa kiusalama na kiulinzi wa Tel Aviv na kusisitiza kuwa, huenda kipigo cha kwanza kikali dhidi ya utawala huo kikawa cha mwisho.
Ametaja baadhi ya matukio hayo kuwa kushambuliwa meli kadhaa za mizigo za utawala huo, mbali na mripuko mkubwa ulioshuhudiwa mwezi uliopita katika kituo cha nyuklia cha siri cha Dimona cha utawala huo haramu.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria hatua ya hivi karibuni ya Marekani kuanza kuwaondoa wanajeshi wake nchini Afghanistan na kubainisha kuwa, "Marekani imeanza kuondoka katika eneo la Asia Magharibi hatua kwa hatua kutokana na irada ya mataifa ambayo ardhi zao zimekaliwa kwa mabavu kwa miaka mingi na Washington."
Jenerali Salami ameongeza kuwa, kambi ya muungano wa kishetani duniani inasambaratika kwa kasi, na kwamba jukumu la Kikosi cha Quds cha jeshi la SEPAH ni kuishinda Marekani. Amesema utawala wa Washington unaandamwa na mashinikizo ya kisiasa, kijamii, upinzani wa fikra za waliowengi na mawimbi makali ya makundi ya muqawama.