Waziri wa Saudi Arabia: Tuna matumaiani na mwenendo wa mazungumzo na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i70316-waziri_wa_saudi_arabia_tuna_matumaiani_na_mwenendo_wa_mazungumzo_na_iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amesema kuwa, nchi yake ina matumaini na mwenendo wa mazungumzo kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 19, 2021 06:54 UTC
  • Waziri wa Saudi Arabia: Tuna matumaiani na mwenendo wa mazungumzo na Iran

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia amesema kuwa, nchi yake ina matumaini na mwenendo wa mazungumzo kati ya nchi yake na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Faisal bin Farhan ameeleza kwamba, mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh yamo katika hatua za awali.

Waziri huyo wa Mashauri ya Kigeni wa Saudi Arabia ameongeza kuwa, kuweko ushirikiano chanya na majirani kunapelekea kupatikana amani, uthabiti na ustawi wa eneo hili la Asia Magharibi.

Mwezi uliopita wa Aprili, Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia alinukuliwa akisema kwamba, Iran ni nchi jirani; na Riyadh ina matumaini kwamba itaweza kuwa na uhusiano mzuri na Tehran.

Mohammad bin Salman, mrithi wa ufalme wa Saudi Arabia

 

Kufuatia matamshi hayo, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ikatangaza kuwa, inakaribisha kwa mikono miwili hatua ya Saudia ya kubadilisha lugha yake kuhusu Iran na kwamba, kwa kuweko mazungumzo mazuri nchi mbili hizi muhimu katika eneo zinaweza kuweka kando hitilafu zao na kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano.

Mnamo mwaka 2016, Saudia ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran. Katika kipindi chote cha miaka mitano iliyopita, Iran imetangaza mara kadhaa kuwa iko tayari kufufua uhusiano wake na Saudi Arabia, lakini Riyadh imekuwa ikipiga upatu wa kuendeleza mvutano na Tehran.

Ripoti mbalimbali zinaonyesha kuwa, kumekuweko na mazungumzo baina ya Iran na Saudia kwa usimamizi wa Iraq ingawa bado haijafahamika hatua iliyopigwa katika mazungumzo hayo.