Maandamano yafanyika Tehran kulaani jinai za utawala wa Israel huko Ghaza
Maandamano yamefanyika mjini Tehran kulaani jinai zinazoendelea kufanywa na utawala katili wa Israel dhidi ya Wapalestina wasio na hatia katika Ukanda wa Ghaza.
Kwa mujibu wa taarifa, maandamano hayo yamefanyika katika Medani ya Imam Hussein AS mjini Tehran ambapo washiriki kutoka matabaka mbalimbali walikuwa wamebeba bendera za Palestina ili kueleza mfungamana wao na taifa hilo linalokandamizwa. Waandamanaji hao pia walisikika wakitoa nara kama: "Mauti kwa Marekani", "Mauti kwa Israel", kama njia ya kueleza hasira zao kwa jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Mijumuiko kama hiyo imefanyika pia katika miji mingine ya Iran kuwaunga mkono Wapalestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.
Iran imekuwa mstari wa mbele kuwatetea watu wa Palestina ambao wamekuwa wakikandamizwa kwa zaidi ya miaka 70 baada ya ardhi zao kuporwa na Wazayuni ambao waliasisi dola bandia la Israel.
Jana Spika wa Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alikosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa, asasi za kibinadamu na Umoja wa Mataifa mbele ya jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina.
Muhammad Baqir Qalibaf aliyasema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Marzouq Ali al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait ikiwa ni mwendelezo wa mazungumzo yake na maspika wa mataifa ya Kiislamu kuhusiana na hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Israel huko katika Ukanda wa Gaza.
Katika mazungumzo yake hayo, Spika wa Bunge la Iran ameashiria unyama na jinai za Israel zisizo na kikomo zinazofanyika kwa himaya na msaada wa Marekani na kueleza kwamba, hii leo maumivu ya mataifa ya Kiislamu ni kumwagwa damu za wanawake na watoto wadogo wa Kipalestina.
Naye Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema, kwa kuivuka Intifadha ya kupambana kwa mawe na kuingia kwenye Intifadha ya kupambana kwa makombora, wananchi mashujaa wa Palestina wameigeuza ndoto ya Wazayuni ya kutawala kuanzia Mto Nile hadi Mto Furati (Euphrates) kuwa jinamizi la kupigania kuilinda kambi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.