Ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kurejea katika umaanawi na maadili mema
-
Sayyed Hassan Khomeini
Ujumbe muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kutoa wito kwa dunia ya sasa irejee katika umaanawi na maadili mema.
Hayo yamesemwa na mjukuu wa Imam Khomeini -Mwenyezi Mungu Amrehemu-, Hujjatul Islam Sayyed Hassan Khomeini Alkhamisi alipohutubu katika Kongamano la Kimataifa la 'Imam Khomeini na Ulimwengu wa Kisasa". Kongamano hilo limefanyika kwa mnasaba wa kukumbuka mwaka wa 32 wa kuaga dunia Imam Khomeini MA, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Amesisitiza kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu miaka 43 iliyopita haukuwa na taathira katika mipaka ya Iran tu bali ujumbe wake ulifika katika nchi za Kiislamu na zisizo za Kiislamu.
Sayyed Hassan Khomeini ameongeza kuwa Mapinduzi ya Kiislamu yaliirekebisha jamii na kulea wanasayansi katika vijiji sambamba na kulea kizazi kipya ambacho kimeinukia na mafunzo ya Imam Khomeini MA.
Halikadhlika amesema Imam Khomeini aliweza kulifanya taifa la Iran lishikamane zaidi na dini na kuongeza kuwa, 'moja ya turathi muhimu za Imam Khomeini ni Jamhuri ya Kiislamu'. Aidha amesema ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yakiongozwa na Imam Khomeini, uliashiria kuangamia daima mfumo wa ufalme nchini Iran.