Wiki ya Imam Khomeini yaadhimishwa nchini Nigeria
Wanafunzi Waislamu wa Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu za Nigeria wameandaa Wiki ya Imam Ruhullah Khomeini, mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika jimbo la Bauchi, kaskazini mashariki mwa nchi.
Maadhimisho hayo yameandaliwa na Jukwaa la Akademia, ambalo linawajumuisha wanachuo Waislamu wa Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu za nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Katika vikao hivyo, wahadhiri na wasomi Waislamu wamezungumza kuhusu maisha na mafanikio ya Imam Khomeini (MA). Miongoni mwa wasomi mashuhuri waliohutubu katika vikao hivyo vya Wiki ya Imam Khomeini, ni Sheikh Ahmad Yusuf Yashi.
Aidha mashairi na tungo za kumsifu Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimewasilishwa katika vikao hivyo.

Moja ya tungo hizo za kumsifu Imam Ruhullah Khomeini, na iliyowasilishwa kwa lugha ya Kihausa inasema "Ewe Allah Mtukufu, Mrehemu Imam Khomeini, na umpeleke aliko Mtume Muhammad (SAW).
Ijumaa iliyopita ya tarehe 4 Juni, mwafaka na tarehe 14 Khordad kwa mwaka wa Hijria Shamsia, ilisadifiana na mwaka wa 32 wa kufariki dunia Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran, Imam Ruhullah Khomeini.