Uchaguzi wa Rais wa Iran kufanyika London, miji mingine 6 ya Uingereza
Ubalozi wa Iran nchini Uingereza umesema wananchi wa Iran walioko katika nchi hiyo ya bara Ulaya watakuwa na fursa ya kupiga kura katika uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu katika mji mkuu London, na miji mingine sita mikubwa ya nchi hiyo.
Taarifa ya ubalozi huo imesema kuwa, vituo 11 vya kupigia kura vitawekwa nchini Uingereza, ambapo vitano vitakuwepo jijini London, huku kituo kimoja kimoja kikiwekwa katika miji ya Manchester, Birmingham, Leeds, Glasgow, Cardiff na Newcastle.
Iwapo italazimu, na kwa mashauriano na Bodi Kuu ya Uchaguzi ya Iran, muda wa upigaji kura huenda ukaongezwa katika baadhi ya vituo nchini Uingereza; kwa kutegemea idadi ya wapiga kura watakaojitokeza.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wananchi wa Iran walioko Uingereza watahitajika kuwa na vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa au pasipoti zenye itibari ili waruhusiwe kushiriki zoezi hilo la kidemokrasia.
Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya wiki ijayo ya tarehe 18 mwezi huu wa Juni, 2021 ndani na nje ya nchi. Wagombea urais katika uchaguzi huo ni Saeed Jalili, Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi, Alireza Zakani, Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, Mohsen Mehralizadeh na Abdolnaser Hemmati.
Wagombea hao wa Urais wanaendelea kunadi sera zao katika majukwaa mbalimbali, na kesho Jumamosi wanatazamiwa kushiriki katika Mdahalo wa tatu na wa mwisho wa urais.