Usalama umeimarishwa nchini Iran kuelekea uchaguzi mkuu wa kesho
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71348-usalama_umeimarishwa_nchini_iran_kuelekea_uchaguzi_mkuu_wa_kesho
Vyombo vya dola nchini Iran vimesema kuwa usalama umeimarishwa kote nchini kuelekea Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu unaofanyika kesho Ijumaa.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 16, 2021 22:34 UTC
  • Usalama umeimarishwa nchini Iran kuelekea uchaguzi mkuu wa kesho

Vyombo vya dola nchini Iran vimesema kuwa usalama umeimarishwa kote nchini kuelekea Uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu unaofanyika kesho Ijumaa.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran, Ali Rahmani Fazli amesema maafisa usalama wapatao milioni moja na laki tano wameenezwa katika pembe zote za nchi ili kuwadhaminia usalama wananchi wa Iran katika kipindi hiki cha kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi.

Amesema vyombo vya usalama vimesambaratisha njama zote za maadui za kujaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi huu. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran ameongeza kuwa, vituo vya kupigia kura vitafungulia mwendo wa saa moja asubuhi hadi saa sita adhuhuri, na yumkini muda wa upikaji kura ukasogezwa mbele hadi saa nane usiku, kwa kutegemea idadi ya wapigakura watakaojitokeza.

Amekumbusha kuwa, watazamaji 70, 000 wa uchaguzi wanalifuatilia zoezi hili la kidemokrasia kwa karibu, ambapo Wairani zaidi ya milioni 59 wametimiza masharti yote ya kupiga kura.

Saeed Jalili, wa punde kuiondoa kwenye Uchaguzi wa Rais Iran

Huku hayo yakiarifiwa, Sa’eed Jalili amekuwa mgombea wa tatu kujiondoa kwenye kinyang'anyiro cha urais. Katika taarifa jana jioni, Jalili amewaomba wafuasi wake wenye imani na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979 wampigie kura Sayyid Ebrahim Raeisi. Mapema jana, Alireza Zakani na Mohsen Mehralizadeh walitangaza pia kujiondoa kwenye uchaguzi huo unaotazamiwa kuwa na ushindani mkali.

Wagombea waliosalia katika kinyang'anyiro hicho cha Ijumaa ya kesho ni pamoja na Mohsen Rezaee Mirgha'ed, Sayyid Ebrahim Raisi,  Sayyid Amir-Hossein Ghazizadeh Hashemi, na Abdolnaser Hemmati.

Uchaguzi wa 13 wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatarajiwa kufanyika Ijumaa ya kesho ya Juni 18  ndani na nje ya nchi. Rais wa sasa Hassan Rouhani anayemaliza muhula wake wa pili mfululizo haruhusiwi kugombea urais katika awamu hii.