Iran yalaani kushambuliwa wapigakura katika nchi za nje
Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran limelaani vikali vitendo vya kushambuliwa na kuhujumiwa raia kadhaa wa Jamhuri ya Kiislamu waliojitokeza kupiga kura jana Ijumaa katika nchi kadhaa za Magharibi.
Katika ujumbe wa Twitter uliotumwa usiku wa kuamkia leo, baraza hilo limesema Wairani kadhaa waliojitokeza katika ofisi za kibalozi za Jamhuri ya Kiislamu katika nchi za Uingereza, Australia na New Zealand walishambuliwa, licha ya uwepo wa maafisa wa polisi wa nchi hizo.
Duru za habari zinaarifu kuwa, magenge ya watu wanaopinga Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ndio waliohusika na hujuma hizo dhidi ya wapigakura wa Kiirani ughaibuni.
Taarifa ya Baraza Kuu la Haki za Binadamu la Iran limeongeza kuwa: Nchi hizo (Uingereza, Australia na New Zealand) pamoja na Canada ambayo ilikataa Wairani karibu nusu milioni wanaoishi nchini humo kupiga kura; zote zinapokea amri kutoka 'ofisi ya kifalme.'
'Ofisi ya kifalme' inayozungumziwa katika ujumbe huo wa Twitter wa Baraza la Haki za Binadamu la Iran ambalo liko chini ya Vyombo vya Mahakama vya nchi hii, inajumuisha familia na waungaji mkono wa tawala za kidikteta na kifalme zilizoongoza Iran kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.
Zaidi ya Wairani milioni 59 waliokuwa wametimiza masharti ya kupiga jana walijitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa rais ambao ulikuwa wa wagombea wanne baada ya Wagombea wengine watatu kujiondoa katika mchuano huo Jumatano.
Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Sayyid Ebrahim Raeisi amepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliofanyika jana Ijumaa.