Iran yazima jaribio la kushambuliwa shirika lake la nishati ya atomiki
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i71596-iran_yazima_jaribio_la_kushambuliwa_shirika_lake_la_nishati_ya_atomiki
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetibua njama za kuhujumiwa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya nchi hii mjini Karaj, nje kidogo ya mji mkuu Tehran.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 23, 2021 22:36 UTC
  • Iran yazima jaribio la kushambuliwa shirika lake la nishati ya atomiki

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetibua njama za kuhujumiwa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya nchi hii mjini Karaj, nje kidogo ya mji mkuu Tehran.

Taarifa ya Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran (AEOI) imesema jaribio hilo la mapema jana Jumatano la kukishambulia kituo cha shirika hilo mjini Karaj limezimwa, na wala hakuna uharibifu wowote ulioripotiwa.

Imeongeza kuwa, hatua madhubuti za kiusalama katika taasisi hiyo ya nishati ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu zimepelekea kugonga ukuta njama hizo za maadui wa taifa la Iran.

Taarifa ya Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran imebainisha kuwa, uchunguzi wa kubaini wahusika wa njama hizo umeanzishwa.

Ikumbukwe kuwa, Aprili mwaka huu, sehemu moja ya umeme ya taasisi ya urutubishaji urani ya Shahid Ahmadi Roushan katika kituo cha nyuklia cha Natanz hapa nchini Iran ilihujumiwa.

Kituo cha nishati ya nyuklia cha Natanz

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulijigamba kuwa ndio uliofanya uharibifu huo huku vyombo vya habari vya Magharibi vikilivalia njuga mno suala hilo mpaka kufikia kudai kuwa eti urutubishaji urani nchini Iran utasimama kwa miezi kadhaa kutokana na uharibifu huo.

Hata hivyo Dk Ali Akbar Salehi, Mkuu wa Taasisi ya Nishati ya Atomiki ya Iran alisisitiza kuwa, uharibifu huo haukuathiri zoezi hilo na urani iliyorutubishwa kwa asilimia 60 tayari imeanza kuzalishwa.